Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amewataka viongozi wa dini kukemea maovu katika jamii, ikiwemo mmomonyoko wa maadili.
Akizungumza na viongozi wa dini waliofika Ikulu jijini Dar es salaam, Rais Magufuli amesema kwamba inafahamika kuwa watu wasiovaa mavazi ya heshima hawaruhusiwi kuingia kanisani, lakini itakuwa vyema kama watu hao hawataruhusiwa kuingia sehemu yoyote.
Akizidi kufafanua hilo Rais Magufuli amesema anavutiwa na kanisa la Askofu Kakobe wanavyofunga viremba, kwani hayo ndio maadili ya Mtanzania.
“Najua Roman Catholic wanaweka matangazo kuwa wenye nguo zisizo na heshima hawaruhusiwi kuingia kanisani, sasa tuende mbali na hapo, tusizungumze tu wasiruhusiwe kuja kanisani, wasiruhusiwe mahali popote, ndio maana nafurahi kanisa la mzee Kakobe wanafunga na vitambaa wote, hawataki kuonekana nywele ingawa nywele za Kakobe huwa tunaziona”, amesema Rais Magufuli.
Hii leo Rais Magufuli amekutana na viongozi wa Dini Ikulu jijini Dar es salaam, kujadili changamoto mbali mbali zinazowakabili kwenye sekta yao.
Social Plugin