Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Antiphas Lissu amemlalamikia Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kwa kushindwa kutimiza ahadi yake ya kwenda kumuona hospitalini kama alivyoahidi.
Lissu ameyasema hayo kupitia Waraka huo wenye kichwa cha habari ‘Mwaka mpya 2019, Mwaka wa kurudisha demokrasia, haki za binadamu na utu wetu Tanzania’ .
Lissu amelalamika kutotembelewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai wala watumishi wa Bunge licha ya kuahidiwa.
“Kabla sijahamishiwa nchini Ubelgiji (Januari 6 mwaka jana) kutoka Kenya, Spika Ndugai aliahidi hadharani, kwenye mahojiano na Azam TV, kwamba atafika kunitembelea, mahali popote nitakapokuwa nimelazwa hospitalini.
"Hadi ninapoandika maneno haya, bado Spika Ndugai hajatimiza ahadi yake hiyo. Hakuna mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge, au ofisa yeyote wa Bunge, aliyefika hospitalini kuniona na kunijulia hali.”
Akizungumzia kuhusu madai hayo, Spika Ndugai amesema wameshayatolea ufafanuzi malalamiko hayo mara kadhaa.
Amesema alipanga kwenda kumtembelea Nairobi lakini, “tarehe zangu nilizokuwa nimezipanga, akawa amehamishiwa kwenda Ubeligiji, kwa hiyo safari yote ikawa imevurugika.”
Kuhusu Bunge kugharamia matibabu yake, alisema ni kwa sababu hakufuata utaratibu unaotakiwa kwa mbunge kutibiwa nje.
“Mbunge hatibiwi katika nchi anayotaka mwenyewe kama yeye anavyofanya, unatibiwa nje pale inapobidi, pale unapokuwa na recommendations (ushauri) ya madaktari bingwa watatu wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema.
Alisema kuna wabunge wanaotibiwa nchi za mbali kama Ujerumani, Uingereza na Marekani kwa gharama zao.
“Sasa nashangaa analalamika kitu gani wakati ukishachagua jambo si unaenda na chaguo lako?” alihoji.
Aliongeza kuwa Bunge linaendelea kumlipa mshahara kwa sababu hajafukuzwa kazi.
“Tumempenda sana huko aliko na ndiyo maana anauliza kwa nini tunaendelea kumlipa, angesema ahsante kwa upande huo, angalau mmenijali,” alisema.
Aidha, Tundu Lissu amelalamika tangu kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa risasi Septemba 7, 2017 hakuna mtu yoyote aliyehojiwa na wapelelezi wala Jeshi la Polisi kutofanyia uchunguzi shambulio hilo.
“Katika shambulio hili, hakuna anayeshukiwa na Jeshi letu la Polisi hadi sasa. Hakuna aliyehojiwa na wapelelezi mahiri wa Jeshi letu la Polisi. Hakuna aliyekamatwa na kwa hiyo, hakuna aliyeshtakiwa” alidai Lissu.
Hata hivyo, Oktoba 2017, akizungumza na vikosi vya jeshi hilo Mbeya, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro alitangaza kufunga mjadala kuhusu kupigwa risasi kwa Lissu huku akiwaonya wanasiasa kuacha kuuendeleza na waliachie jeshi lifanye kazi yake.
Katika waraka wake huo, Lissu amesema anaendelea vizuri na matibabu, kwa sasa ameanza mazoezi ya kutembea bila magongo.