Rais John Magufuli jana alieleza jinsi alivyosoma meseji za watendaji wake serikalini na kubaini baadhi yao wanagombana badala ya kufanya kazi kwa ushirikiano katika maeneo yao.
Alisema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam jana baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua.
Alitoa mfano jinsi alivyosoma meseji za majibizano kati ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, (Tamisemi), Zainabu Chaula ambaye jana aliapishwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya.
“Nilikuwa nazisoma meseji; meseji ya Waziri wa Afya na meseji ya Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi, wanajibizana wee na wote wanatoka Tanga. Huyu mwingine anakaa kimya, huyu mwingine anashindilia maneno, nikaona nani anashindiliwa maneno zaidi, nikasema hawa njia ya kuwakomesha niwaweke wizara moja,” alisema Rais Magufuli.
Alisema wote wawili wanafanya kazi vizuri, hivyo ameona bora wakae wizara moja. Alimpongeza Chaula kwa jitihada zake za kusimamia ujenzi wa hospitali zaidi ya 300 ndani ya miaka mitatu.
Mbali ya viongozi hao, Rais Magufuli pia alisema anafahamu jinsi watendaji katika baadhi ya halmashauri wanavyogombana. Alitolea mfano Halmashauri ya Nyasa ambako alisema mkurugenzi na mkuu wa wilaya hawaivi.
Alitaja mgogoro mwingine kuwa uko Gairo ambako alisema mbunge wa anagombana na mkuu wa wilaya. Mbunge wa Gairo ni Mbunge wa jimbo hilo Ahmed Shabiby (CCM), na Mkuu wa Wilaya ni Siriel Mchembe.
Alisema mbunge amefikia hatua ya kutuma maneno ya kumtukana DC na kusema anashindwa kuelewa kwamba kuna kamati za nidhamu za CCM ambazo zinaweza kumfanya apoteze ubunge.
“Nimewaangalia tu, I hope (natumai- mbunge) atafika siku moja aombe msamaha kwenye Bunge,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:
“Pale Dodoma, mkurugenzi wa Jiji na DC walikuwa wanagombana, nika-send message (nikatuma ujumbe) kwamba ‘endeleeni kugombana tu, mtagombania vijijini siku moja. Wamenyamaza naona yameisha,”
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma ni Godwin Kunambi na DC ni Patrobas Katambi.
Na Peter Elias, Mwananchi
Social Plugin