Mahakama ya kikatiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Jumapili imemtangaza Felix Tshisekedi kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais na kutupilia mbali madai ya Fayulu kwamba uchaguzi huo ulikuwa na udanganyifu.
Uamuzi huo wa kuthibitisha kuwa Tshisekedi ndiye aliibuka mshindi wa kinyang'anyiro hicho cha urais unakuja baada ya mahakama kupinga kesi iliyowasilishwa na kiongozi wa muungano wa upinzani wa LAMUKA Martin Fayulu, licha ya kuwa na mashaka makubwa ya kuwepo udanganyifu wa kura.
Fayulu anadai kwamba Tshisekedi na Rais Joseph Kabila walifanya mpango wa kisiri siri baada ya matokeo ya awali kuonesha kwamba mgombea ambaye alikuwa akiungwa mkono na Kabila, Emmanuel Ramazani Shadary, ameshika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo.
Uamuzi huo wa mahakama unamaanisha kuwa sasa Tshisekedi anaweza kuapishwa kuwa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ifikapo Jumanne wiki ijayo.
Fayulu ameitaka jumuiya ya kimataifa kupinga ushindi huo wa Tshisekedi kwa kutotambua mamlaka yake aliyoyataja yasiyoungwa mkono na Wacongo. Fayulu amejitangaza kuwa Rais halali wa Congo.
Vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa siku ya Jumanne viliripoti kuwa data zilizovujishwa za uchaguzi wa Congo zilionesha kuwa Fayulu ndiye aliyeshinda na sio Tshisekedi.
Kanisa lenye ushawishi mkubwa nchini Congo la Kikatoliki pia limeunga mkono hoja ya Fayulu kuwa Tshisekedi hakushinda katika uchaguzi huo wa Desemba 30 na Umoja wa Afrika ulitaka matokeo kamili ya uchaguzi huo wa Rais kucheleweshwa.
Nchi za magharibi bado hazikumpongeza Tshisekedi
Nchi za magharibi bado hazikumtumia pongezi Tshisekedi, na Ufaransa imeeleza wasiwasi wake juu ya matokeo rasmi ya uchaguzi, ambayo yamempatia ushindi Tshisekedi kwa asilimia 38.57 ya kura zote zilopigwa na Fayulu kupata asilimia 34.8.
Gazeti la Financial Times na vyombo vengine vya habari vya kimataifa vimethibitisha kuona nyaraka zinazosema kuwa Fayulu ndiye mshindi wa uchaguzi huo.
"Iwapo mahakama itamtangaza Tshisekedi mshindi, hatari ya taifa hilo kutengwa ni kubwa kwa taifa mabalo lipo katikati ya bara la Afrika," Adeline Van Houtte wa kampuni ya utafiti wa kiuchumi ya Economist Intelligence Unit, ameandika katika ukurasa wa Twitter.
Kambi ya Fayulu iliusifu Umoja wa Afrika kwa kutoa ombi la kutaka matokea ya mwisho yaahirishwe, lakini kambi ya Tshisekedi ilisema ni ombi litakaloleta kashfa.
Mvutano huo umezua wasiwasi kwamba mgogoro wa kisiasa ulioanza mara baada ya Rais Joseph Kabila kukataa kuachia madaraka mwishoni mwa muhula anaoruhusiwa kikatiba kumalizika miaka miwili iliyopita unaweza kusababisha umwagaji damu mkubwa.
Taifa hilo kubwa barani Afrika na ambalo limekosa utulivu kwa muda mrefu, lilitumbukia katika vita vya kikanda 1996-97 na 1998-2003, na chaguzi mbili zilizopita, 2006 na 2011 zilighubikwa na mapigano ya umwagaji damu.
Umoja wa Afrika umechukua msimamao mkali miongoni mwa mashirika yote ya kimataifa kuhusu fujo zinazoweza kuzuka kufuatia uchaguzi nchini humo.
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika-SADC, ambayo inajumuisha Angola na Afrika Kusini awali ilitoa wito wa kura kuhesabiwa tena pamoja na kuundwa kwa serikali ya umoja wa muungano.
Lakini taarifa yake ya baadaye, haikutaja madai hayo, badala yake iliwatolea wito wanasiasa wa Congo "kushughulikia malalamiko yoyote ya uchaguzi kulingana na Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na sheria husika za uchaguzi".
Credit:DW
Social Plugin