Vyama 10 vya upinzani nchini Tanzania kupitia muungano wao vimefungua kesi Mahakamani Kuu ya Tanzania kupinga muswada wa sheria ya vyama vya siasa kujadiliwa na Bunge kwa ajili ya kuupitishwa kuwa sheria.
Kesi hiyo imefunguliwa Desemba 20,2018 ikitarajiwa kuanza kusikilizwa kesho Ijumaa Januari 4,2019 huku mlalamikiwa akiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akisoma tamko la umoja huo leo Alhamisi Januari 03, 2019, Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe amesema muswada huo unakinzana na Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 hivyo ni muhimu kwao kuupinga.
“Serikali imepeleka bungeni muswada wa sheria ya vyama vya siasa unaohalalisha agizo la Rais Magufuli alilolitoa mkoani Singida mwaka 2016 kuzuia mikutano ya vyama vya siasa. Muswada huu unafanya shughuli za kisiasa kuwa suala la jinai.
“Tumefungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar chini ya hati ya dharura kupinga Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa kujadiliwa na Bunge kwa minajiri ya kuupitisha kuwa sheria kwa sababu unakinzana na katiba ya nchi.
"Hatuwezi kwenda kuujadili Bungeni, mnajua kuna wabunge wengi wa CCM, baadhi yao ni wazuri na tumekuwa tukijadiliana nao, lakini wengine ni makasuku. Kuna wabunge wengine wa CCM wanapenda sifa, siyo kwamba utakuwa mbaya tu lakini utatoka mbaya zaidi.
“Muswada huo unalenga kumfanya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa na Mamlaka ya Usimamizi (Regulatory Authority), kuwa na mamlaka ya kuingilia shughuli za kiutawala na maamuzi ya ndani ya vyama vya siasa ikiwemo kusimamisha/ kumfukuza mtu uanachama,” amesema Zitto Kabwe.
Social Plugin