Mwili wa mkazi wa kitongoji cha Mbomai wilayani Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro, Florid Lazari umefukuliwa na polisi na kukutwa nusu yake ukiwa umewekwa kwenye mfuko maarufu kama kiroba.
Tukio hilo limekuja siku chache baada ya mwili mwingine kufukuliwa katika kijiji cha Mpinji, kata ya Mamba wilayani Same mkoani humo na kubainika kuwa ni wa mwalimu Alison Mcharo aliyetoweka mwaka 2006.
Jeshi la Polisi linamshikilia mkewe, Nasemba Alison (80) na mwanaye Orgenes Alison (45) kwa mahojiano na taarifa za awali za polisi zinadai mkewe alikiri kuhusika na mauaji ya Alison.
Hata hivyo, juzi tukio hilo likiwa bado vichwani mwa wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, polisi wilayani Rombo walifukua mwili mwiingine na kutambuliwa kuwa ni wa Lazari aliyetoweka usiku wa Desemba 16, 2018.
Taarifa zinasema usiku huo, watu wasiojulikana walifika nyumbani kwake na kumuita atoke nje na alipotoka hakurudi na hakuonekana hadi taarifa zilipotolewa polisi.
Diwani wa Tarakea Motamburu, Michael Beda alisema mwili huo uligunduliwa umezikwa katika msitu wa Serikali wa Nusu Maili unaopakana na msitu wa Mlima Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa diwani huyo, mwili huo ulipofukuliwa ulibainika kuwa umewekwa kwenye kiroba kuanzia kichwani hadi kiunoni, huku kichwa kikiwa na jeraha la kupigwa na kitu kizito.
Akifafanua zaidi, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Agnes Hokororo alisema taarifa za kutoweka kwa mtu huyo zilitolewa Desemba 17, 2018 na jitihada za kumtafuta hazikuzaa matunda hadi juzi mwili wake ulipofukuliwa.
“Tarehe 1.01.2019 ndio zikapokelewa taarifa kuwa hapo msituni kunaonekana kama kuna kitu kimefukiwa, kwa hiyo kukawa na hisia huenda ni mwili wa huyo mtu aliyepotea,” alisema.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, polisi walifika eneo hilo na kulizungushia uzio na kisha taratibu za kuomba kibali cha mahakama zilifanyika na kibali cha kufukua kikapatikana hiyo juzi.
“Kwa hiyo lile eneo lilipofukuliwa ndio ukakutwa huo mwili japo ulikuwa umeharibika sana. Ndugu waliutambua na waliuchukua siku ileile kwenda kuuzika upya nyumbani kwake.”
Alisema, “Sasa kuhusu nani ni mhusika wa mauaji yale, ilikuwaje na kwa nini afanye unyama wote ule hilo nawaachia polisi kwa sababu wao ndio mamlaka ya uchunguzi wa matukio hayo.”
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Hamis Issah jana alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa watu kadhaa wanashikiliwa na jeshi hilo wakiwamo baadhi ya ndugu wa marehemu.
Na Daniel Mjema na Florah Temba mwananchi
Social Plugin