Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ANAYEDAIWA KUUA MWALIMU AFIKISHWA MAHAKAMANI


Mtuhumiwa Seif Salimu anayedaiwa kuhusika na mauaji ya mwalimu wa Shule ya Msingi ya Mailisita Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Dinna Lekule, miaka 12 iliyopita amekamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Hai.

Mwendesha Mashtaka, Meja Lebulu Mbise aliiambia mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Devota Msofe kuwa mshtakiwa Salimu, maarufu kwa jina la Sharifu, alitenda kosa hilo usiku wa Agosti 21, 2007 nyumbani kwa marehemu Mailisita.

Hata hivyo, mshtakiwa ambaye ni mkazi wa kijiji cha Doma Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, hakutakiwa kujibu lo lote katika kesi hiyo, ambayo aliiahirisha hadi Januari 21, mwaka huu itakapotajwa tena.

Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, mume wa marehemu, Dk Redfan Shao wa Hospitali ya Wilaya ya Hai, alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo.

Alisema kutokana na tukio hilo, alikamatwa na kuwekwa mahabusu kwa miezi 10, akituhumiwa kumuua mkewe.

Alisema, hata hivyo, siku ya tukio hilo alikuwa Handeni katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni kikazi.

Alisema, baada ya tukio hilo alipigiwa simu na kurejea nyumbani Agosti 22 na kujikuta akitiwa mbaroni, akihusishwa na mauaji hayo.

 Dk Shao alisema, baada ya upelelezi Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mahakama, walijiridhisha kuwa hakuhusika na mauaji hayo na kumwachia huru baada ya miezi 10 na sasa anaendelea na kazi katika Hospitali ya Wilaya ya Hai.

Akisimulia kifo cha mkewe, Dk Shao alisema, marehemu alipigwa na kitu chenye ncha kali kichwani, alivunjwa mkono wa kushoto mara mbili na kuchomwa na kitu chenye ncha kali kifuani.

Alisema, vitu kadhaa viliibiwa katika nyumba yake ikiwamo televisheni moja aina ya Panasonic, redio, vifaa vya kompyuta na pasi ya umeme.

Na Nakajumo James - Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com