Mwanamuziki wa nyimbo za mtindo wa rap ambaye pia amekuwa mtetezi mkubwa wa haki za wapenzi wa jinsia moja ameuawa kwa kupigwa risasi mara kadha katika jimbo la Puerto Rico akiwa na miaka 24.
Kevin Fret, ambaye amekuwa akielezwa kama mwanamuziki wa kwanza wa nyimbo za mtindo wa Latin Trap kutangaza hadharani kwamba ni mpenzi wa jinsia moja, aliuawa katika mji mkuu wa jimbo hilo wa San Juan Alhamisi, polisi wamesema.
Fret alipigwa risasi mara nane alipokuwa anaendesha pikipiki katika barabara moja mjini humo.
Uchunguzi unaendelea.
Mauaji yake yanafikisha hadi 22, idadi ya watu waliouawa kwa kushambuliwa Puerto Rico mwaka huu kwa mujibu wa polisi.
Meneja wa mwanamuziki huyo Eduardo Rodriguez, amemweleza rapa huyo kwama mwenye moyo wa sanaa na kusema aliupenda sana muziki.
Akithibitisha kifo chake, Bw Rodriguez amesema: "Hakuna maneno yanayoweza kueleza hisia zetu na uchungu unaotulazimisha kukubali uhalisia kwamba mtu mwenye ndoto nyingi ametuacha.
"Ni lazima sote tuungane katika wakati huu mgumu, na kuombea amani kwa Puerto Rico yetu tunayoipenda."
Video ya muziki ya karibuni zaidi ya mwanamuziki huyo kwa jina Soy Asi imetazamwa zaidi ya mara nusu milioni katika mtandao wa YouTube.
"Mimi ni mtu asiyejali wanayoyasema wengine," alikuwa ameambia jarida la mtandaoni kwa jina Paper mwaka jana.
"[Siku hizi nawaona] vijana wapenzi wa jinsia moja ambao wananitazama kama mfano kwao, wanasema, iwapo yeye alifanikiwa, na hajali yale wasemayo wengine, mimi naye ninaweza."
Puerto Rico imeshuhudia ongezeko la visa vya uhalifu mijini wiki za karibuni.
Polisi wameeleza kisiwa hicho cha Caribbean kama kinachokabiliwa na "mzozo wa ghasia na uhalifu."
Chanzo - BBC
Social Plugin