Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amemwonya aliyekuwa mgombea wa uenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mwanza, Said Meck Sadiki kuacha kuendeleza fitina na badala yake ashirikiane na mshindi halali wa kiti hicho, Anthony Diallo kujenga chama.
Onyo hilo alilitoa jana wakati akizungumza na wajumbe wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM, Mkoa wa Mwanza ambacho kiliwahusisha pia watendaji wa serikali ngazi ya mkoa, wilaya na halmashauri kuangalia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi.
Baada ya hotuba yake hiyo, Dk. Bashiru aliwaita Diallo na Sadick mbele ya wanachama na kuwataka kupeana mikono ya heri na kukumbatiana ikiwa ni ishara ya kuondoa tofauti zao na kuwa kitu kimoja ili mkoa uweze kuwa imara na kushinda uchaguzi ujao.
Dk Bashiru alisema, Sadick alifikisha malalamiko ya kumpinga Dk Diallo ambapo kila mmoja alisikilizwa na uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM iliamuru aliyeshinda uchaguzi wa mwaka jana awaongoze.
Alisema viongozi hao walielezwa kuwaunganisha wanachama kukiimarisha chama na kukinadi kwa wananchi wazidi kukiunga mkono lakini Meck Sadiki ameendeleza fitina za chini chini, jambao ambalo ni hatari kwa ustawi wa chama hicho.
Alisema anatambua Meck Sadik na Dk Dialo ni marafiki lakini wanagawanywa na wanachama na makada ambao dhamira yao washindwe kushirikiana na viongozi kusimamia maendeleo ya wananchi, hivyo aliwaonya kwa pamoja kuachana na tofauti hizo.
“Tukiendekeza migogoro na makundi ya watu hatutafika salama maana tutatoa mwanya kwa watu kufanya ubinafsi kwa maslahi yao.
“Kwanza kinachoendelea kati ya Dk Diallo na Sadick ni sawa na kukidhalilisha chama na wananchi, hali ambayo husababisha kukichukia na kukiadhibu kwenye baadhi ya maeneo,” alisisitiza katibu mkuu huyo.
Aidha Dk Bashiru aliwataka viongozi wa chama ngazi ya mkoa na wilaya kutowapokea na kuungana nao kwenye ziara zao mawaziri ambao hawapiti na kujitambulisha kwenye ofisi za chama hicho na pengine hata kuelezwa kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Awali Dk Bashiru alitembelea na kukagua shamba la ekari 29.23 la CCM lililopo Kijiji na Kata ya Katunguru Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza ambapo alipendekeza kijengwe chuo cha uongozi cha chama ili kusaidia kuelimisha viongozi wa CCM wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Kwa upande wake, Dk Diallo alisema kwamba wamepokea kwa mikono miwili ushauri na maelekezo ya katibu mkuu huyo na watayafanyia kazi ili chama kiwe imara.
Social Plugin