Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amewaomba watanzania kumsamehe Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Antiphas Lissu kwa kauli anazozitoa huko nje ya nchi.
Makonda ametoa kauli hiyo leo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, katika Mkutano wa Wachimbaji, Wafanyabiashara na Wadau wa sekta ya madini nchini.
Makonda amesema kwamba amegundua kwamba kauli za Lissu zinatokana na kwamba bado hajapona vizuri kichwani kutokana na yeye mwenyewe kukiri wakati alipokuwa akimaliza mahojiano katika kipindi cha 'Hard Talk' kilichofanyika jana na kituo cha televisheni cha BBC.
Ameeleza kwamba katika mahojiano hayo, Lissu ameshindwa kujibu juhudi za Magufuli namna anavyopigana katika suala la madini, ambapo aliikimbia mada hiyo na kuzungumzia mambo mengine ya tofauti, hivyo inaonyesha bado anaendelea kupokea malipo.
Aidha katika kusisitizia kauli yake ya kwamba Lissu ni mgonjwa, Makonda amesema kwamba, "Kama bado mgonjwa inamaana kichwani mambo hayajaakaa vizuri na ndo maana anahitaji matibabu na akitoka kule, tunamuomba Spika amfikishe Mirembe pale na aendelee kumuhudumia"
Chanzo : Eatv
Social Plugin