Watoa huduma wa mitandao ya kijamii ya 'Whatsapp' na 'Facebook' wamepunguza kiwango cha kusambaza ujumbe mfupi wa maandishi ambapo sasa mtumiaji hatoweza kusambaza ujumbe kwa watu zaidi ya watano.
Watoa huduma wamefikia hatua hiyo ili kupunguza tabia za watu kuzusha na kuibua taharuki katika mitandao, kupitia taarifa wanazosambaza.
Hapo awali, mtumiaji wa Whatsapp angeweza kupeleka ujumbe kwa watu 20 au makundi zaidi ya moja kulingana na makundi aliyonayo.
Whatsapp, ambayo ina watumiaji wapatao bilioni 1.5, imekuwa ikijaribu kutafuta njia za kuacha matumizi mabaya ya programu, kufuatia wasiwasi wa kimataifa kuwa jukwaa hilo lilikuwa linatumika kueneza habari zisizo na ukweli.