Na Munir Shemweta, RUFUJI
Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula amekerwa na tabia ya wakurugenzi wa halmashauri nchini kuitengea fedha kidogo idara ya ardhi katika halmashauri na hivyo kuifanya idara hiyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani jana, Dk Mabula alisema wakurugenzi wengi katika halmashauri nchini wamekuwa wakiifanya idara ya ardhi kwenye halmashauri hizo kama mtoto yatima.
‘’Ukienda katika halmashauri nyingi idara ya ardhi imekuwa kama mtoto yatima na ofisi zake haziridhishi kabisa ukilinganisha na zile ofisi za idara nyingine kama vile afya na elimu’’ alisema Dk Mabula.
Kwa mujibu wa Dk Mabula, halmashauri nyingi alizotembelea bajeti ya idara ya ardhi haizidi shilingi milioni nne ukiachilia mbali fedha za mapato ya ndani ingawa wakati mwingine hazipatikani zote na kubainisha kuwa tatizo linaloonekana ni wakurugenzi kutofahamu kama idara hiyo ina fedha nyingi na kuweka wazi kuwa iwapo halmashauri zitaamua kuisimamia sekta hiyo kikamilifu zitajikusanya mapato mengi ukilinganisha na sekta nyingine.
Hata hivyo, Dk Mabula alisema, katika ukusanyaji mapato ya serikali nchini sekta ya ardhi inaweza ikawa sekta ya pili au ya tatu kwa kuingiza mapato mengi Serikali ikiwa nyuma ya taasisi zinazoingiza mapato mengi kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji Mashaka Abdallah alimueleza Dk Mabula kuwa idara yake inakabiliwa na changamoto kubwa ya ufinyu wa bajeti inayotengewa kwa ajili ya kutekeleza kazi za ardhi pamoja na vitendea kazi kama Kompyuta, Printer, Shajala na usafiri.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, hali ya ukosefu wa vitendea kazi inawakatisha tamaa watendaji wa sekta hiyo lakini pia inachangia watendaji hao kutofanya kazi zao vizuri na wakati mwingine kuwalazimu kutumia fedha zao za mfukoni kufanikisha kazi walizopangiwa.
Katika muendelezo wa ziara yake mkoa wa Pwani katika halmashauri za wilaya za Rufiji, Kibiti, Mkuranga pamoja na Kisarawe Dk Mabula alikuta kila halmashauri ikidai kiasi kikubwa cha fedha kwa wamiliki wa viwanja na mashamba tofauti na kiwango ilichowekewa kukusanya kwa mwaka.
Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halamashauri ya wilaya ya Rufiji Mashaka Abdallah alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 halmashauri yake ilipangiwa kukusanya jumla ya shilingi milioni 15 na hadi kufikia tarehe 31 Desemba 2018 ilishakusanya shilingi milioni 16.7 ikiwa ni sawa na asilimia 111.6.
Akigeukia suala la ukusanyaji mapato kupitia sekta ya ardhi, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema halmashauri nyingi zimekuwa zikifanya makisio machache ya fedha za makusanyo inayopangiwa huku zikiacha fedha nyingi kwa wadaiwa na kuwataka watendaji wake kuweka makadirio kulingana na uhalisia wa madeni wanayodai.
Alitolea mfano wa halmashauri ya wilaya ya Rufiji kuwa pamoja na kuwekewa kiwango cha kukusanya shilingi milioni 15 kwa mwaka na kukusanya milioni 16.7 hadi kufikia desemba 2018 na kujivunia kuvuka lengo la mapato lakini kumbukumbu zilizopo Wizara ya Ardhi zinaonesha halmashauri hiyo inadai kiasi cha shilingi bilioni Moja.
Amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuweka mkazo katika makusanyo ya kodi ya ardhi na kubainisha kuwa wakurugenzi hao wangeweza kuzisaidia idara za ardhi kupitia mapato yao ya ndani katika kuzipatia vifaa na ofisi lakini wanashindwa kufanya hivyo na kusisitiza kuwa ni lazima idara hizo ziwezeshwe ili zifanye kazi kwa ufanisi.
Alibainisha kuwa, hata baada ya sasa kuelezwa kuwa asilimia thelathini ya mapato ya halmashauri ambayo yalikuwa yakirejea kwenye halmashauri kuondolewa, wakurugenzi wamekata tama na kuziacha idara hizo bila kuzisaidia lakini wakisahau kuwa mapato yanayopatikana kupitia sekta ya ardhi ndiyo yanayorudi kusaidia shughuli za maendeleo.
Amewataka wakurugenzi wa halmashuri nchini kubadili tabia zao za kuitenga idara ya ardhi na hivyo kuisadia kwa hali na mali kuhakikisha inafanya kazi zake kwa ukamilifu na mwisho wa siku kuisadia kuingiza mapato serikalini.
Amewataka wakurugenzi wa halmashuri nchini kubadili tabia zao za kuitenga idara ya ardhi na hivyo kuisadia kwa hali na mali kuhakikisha inafanya kazi zake kwa ukamilifu na mwisho wa siku kuisadia kuingiza mapato serikalini.
Social Plugin