Bwana mmoja nchini Taiwan amepigwa faini baada ya kumsafirisha paka wake kama kifurushi kwa njia ya mawasiliano ya posta.
Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa habari wa UDN bwana huyo mwenye miaka 33 aliyetambulika kwa jina lake la ukoo la Yang amepigwa faini ya dola za Taiwan NT$60,000 ( sawa na dola za Marekani 1,952) kwa kuvunja sheria ya Ulinzi wa Wanyama ya Taiwan.
Tukio hilo lilitokea wiki iliyopita ambapo bw Yang alimfungasha kwenye kifurushi paka wake aina ya Scottish fold kwenda kwenye kituo kimoja cha kuhifadhi wanyama nchini humo katika wilaya ya Banciao. Yang amedai kuwa hakuwana mahitaji tena ya kuendelea kumfuga paka huyo.
Kutokana na kosa hilo, alilipishwa faini ya ziada ya NT$30,000 kwa kuvunja sheria ya kuzuia na kupambana na magonjwa ya kuambukiza ya wanyama sababu wafanyakazi wa kituo cha wanyama alipopokela paka huyo waligundua kuwa hakupewa chanjo ya kichaa na kuzuia hasira kali.
Maafisa wa ulinzi wa wanyama wa mjini Taipei walifanikiwa kumnasa mtuma kifurushi hicho kupitia kampuni ya posta na mkanda wa kamera za ulinzi za polisi.Mamlaka ya ulinzi wa wanyama inasema paka huyo ana afya njema na baada ya uchunguzi zaidi anaweza kuchukuliwa na mmiliki mpya.
Baada ya kufanya uchunguzi wao, wakamtia mikononi mwao bw Yang ambaye alijitetea kuwa alijaribu kumgawa paka huyo bila ya mafanikio. Yang pia alidai hakuwa na muda wa kutosha wa kumuangalia mnyama huyo na kumtunza. Paka huyo pia ana matatizo ya kutembea baada ya kujeruhiwa, na licha ya kupatiwa matibabu kadhaa, yakiwemo ya kimila bado hali yake haijatengemaa.
Mkurugenzi wa mamlaka ya wanyama, Chen Yuan-chuan, amelaani vikali mkasa huo akisema: "Mnyama anaweza kupatwa na hali mbaya kwa kukosa hewa ndani ya kifurushi na kupandwa na ghadhabu pia hakukuwa na maji safi na salama."
Bw Yuan-chuan amewataka watu kufuata taratibu halali za kisheria pale wanapoona hawawezi tena kuendelea kuwatunza wanyama wao wa nyumbani.
Chanzo- BBC
Social Plugin