Mama na mwanawe mwenye umri wa miezi sita wamefariki dunia papo hapo juzi baada ya kupigwa na radi wakati walipokuwa shambani katika Kijiji cha Msasa,wilayani Geita.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi, Diwani wa Kata ya Busanda, Elias Kisome, aliwataja waliofariki kuwa ni Zainabu William (30) na mwanawe wa kike mwenye umri wa miezi sita, Happiness Bahati.
Akizungumzia mazingira ya tukio hilo, Diwani Kisome, alisema lilitokea saa 10 jioni wakati mama huyo na mwanawe alipokuwa shambani, akipanda mpunga.
Alisema mvua iliyoambatana na radi ilimpiga Zainabu na mwanawe aliyekuwa amembeba mgongoni na kufariki papo hapo.
Oktoba 17 mwaka jana wanafunzi sita wa darasa la pili na tatu katika shule ya msingi ya binafsi ya Emaco Vission English Medium School, iliyopo kata ya Nyankumbu katika Halmashauri ya mji wa Geita walifariki dunia baada ya kupigwa na radi na wengine 23 wakiwamo walimu wawili kulazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Geita.
Chanzo- NIPASHE
Social Plugin