Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la hisani la kimataifa la Oxfam, inaonyesha kuwa mabilionea 26 duniani wanamiliki utajiri ulio sawa na nusu ya binadamu maskini zaidi duniani, na kutaka matajiri watozwe kodi zaidi.
Ripoti hiyo ya Oxfam imetolewa Jumatatu januari 21, 2019, kuelekea kongamano la kimataifa la kila mwaka la kiuchumi litakalofanyika mjini Davos Uswisi. Ripoti hiyo pia inasema mabilionea duniani wameshuhudia utajiri wao ukiongezeka kwa dola bilioni 2.5 kwa siku mwaka 2018.
Watu bilioni 3.8 walio chini ya kiwango, utajiri wao ulishuka kwa asilimia 11 mwaka jana, kwa mujibu wa Oxfam. Shirika hilo limesisitiza kuongezeka kwa pengo baina ya matajiri na maskini, linalochangia kuzorotesha mapambano dhidi ya umaskini, kuharibu uchumi na kuchochea hasira ya umma.
Tajiri namba moja duniani ambaye ni mkurugenzi wa Amazon Jeff Bezoz aliongeza utajiri wake hadi dola bilioni 112 mwaka jana, ambapo asilimia moja ya utajiri wake ni sawa na bajeti nzima ya afya ya Ethiopia, nchi iliyo na wakazi milioni 105.
Mkurugenzi wa Oxfam Winnie Byanyima ametoa akisema, "Watu matajiri duniani, watu walio na nguvu duniani, viongozi wa kisiasa duniani ni lazima wachukue hatua za kupunguza pengo la usawa kwasababu limekithiri. Watu wanaoshiriki kongamano la Davos, viongozi wa makampuni makubwa na viongozi wa kisiasa nao ni sehemu ya tatizo.
Tunawataka waje na suluhisho la kupunguza pengo la usawa, ambalo linazidi kuwa kubwa, linaumiza uchumi, na kudhoofisha demokrasia, hivyo ninatoa wito wa kuchukuliwa hatua ."
Oxfam imeonya kwamba serikali zinazidisha kukosekana usawa kwa kutoboresha huduma za umma kama vile huduma za afya na elimu wakati huo zikiwatoza matajiri kodi kidogo.
Wataalamu wa Oxfam wamekiri kwamba idadi ya watu maskini duniani ilipungua kwa nusu kati ya mwaka 1990 hadi 2010, na tangu wakati huo imeshuka zaidi hadi watu milioni 736. Viwango vya kodi miongoni mwa watu wa kima cha juu vimeshuka katika mataifa tajiri miongo iliyopita.
Shirika hilo linapendekeza kuwa ikiwa watu tajiri duniani watalipa asilimia 0.5 ya ziada katika utajiri wao, itatosha kuwapatia elimu watoto milioni 262 ambao hivi sasa hawahudhurii shule na kutoa huduma za afya na kuokoa maisha ya watu milioni 3.3.
Ripoti hiyo imetolewa leo wakati viongozi wa dunia, matajiri na watu mashuhuri wakiwasili katika mji wa kifahari wa Davos, Uswisi katika kongamano la kila mwaka la kiuchumi.
Social Plugin