Na WAMJW – DOM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Sekta ya Afya nchini yaendelea kukua kwa kasi, kutokana na Serikali kuendelea kuboresha Huduma kwa Wananchi zikiwemo upatikanaji wa Dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi, huduma za chanjo, huduma za afya ya uzazi na mtoto na Huduma za Dharura.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati akitoa tamko mbele ya Waandishi wa Habari na baadhi ya viongozi wa Wizara, kuhusu hali ya Huduma za Afya mwaka 2018, katika ukumbi wa Wizara ya Afya jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema kuwa Katika mwaka 2018, jumla ya wajawazito 2,086, 930 walihudhuria na kuandikishwa Kliniki, ikilinganishwa na wajawazito 2,009,879 Mwaka 2017, huku mwongozo wa utoaji huduma za afya ya uzazi na mtoto unaelekeza wajawazito kuanza huduma mapema kabla ya majuma 12 ya ujauzito na kuhudhuria kliniki angalau mara nne katika kipindi cha ujauzito.
Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa, Katika kipindi cha mwaka 2018 jumla ya watoto 1,568,832 walizaliwa ikilinganishwa na Watoto 1,498,488 mwaka 2017, huku wakipatiwa huduma mbalimbali za chanjo ili kuzuia magonjwa yanayowaathiri Watoto ikiwemo ugonjwa Kupooza, Kuharisha, Pepopunda, Pneumonia, homa ya ini na Surua.
“Katika kipindi cha mwaka 2018 hali ya chanjo kwa Watoto nchini imeendelea kuwa katika kiwango cha juu zaidi ya asilimia 85 ya kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani kama inavyoonyeshaa katik hapa chini” Alisema Waziri Ummy.
Hata hivyo nWaziri Ummy amesema mwaka 2018 kumetokea jumla ya vifo 20,087 ikilinganishwa na vifo 19,693 mwaka 2017, huku Katika kipindi cha miaka yote miwili 2017 na 2018, homa ya mapafu imeongoza kwa kusababisha vifo, ambapo kwa mwaka 2017, imechangia asilimia 18.2 ya vifo vyote na mwaka 2018 imechangia kwa asilimia 12.9 ya vifo vyote.
Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa Mwaka 2018, ugonjwa usio wa kuambukiza (shinikizo la damu) umejitokeza katika magonjwa 10 yanayoongoza kwa kusababisha vifo ambapo umechangia vifo kwa asilimia 1.9 ya vifo vyote.
Kwa upande mwingine, Waziri Ummy amesema kuwa Hali ya upatikanaji wa Dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini imeendelea kuimarika, hii ni kutokana na Serikali kuongeza bajeti ya dawa kutoka Shilingi Milioni 31 mwaka 2015/16 hadi kufikia Shilingi milioni 251 mwaka 2016/17 na Shilingi 270 mwaka 2018/19.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa hali ya upatikanaji wa Damu Salama ambapo katika kipindi cha mwaka 2018, huku jumla ya chupa za damu salama 307,835 sawa na asilimia 85.5 ya lengo zilikusanywa ikilinganishwa na chupa 233,933 mwaka 2017, huku akiwahasa Wananchi kujitokeza kuchangia damu ili kuendelea kuokoa maisha ya wahitaji.
“Chupa zote 307,835 zilizokusanywa zilipimwa makundi ya damu pamoja na magonjwa makuu manne ambayo ni Ukimwi (HIV,) Homa ya Ini B na C (HBV, HCV) na Kaswende (Syphilis). Jumla ya chupa 262,283 sawa na asilimia 85.3 zilikuwa salama na kusambazwa katika hospitali kwa ajili ya wagonjwa wenye uhitaji wa damu.” Alisema Waziri Ummy.
Hata hivyo Waziri Ummy amesema kuwa, katika mwaka 2018 jumla watu 47,967 waligundulika kuwa na vijidudu vya Kifua kikuu ikilinganishwa na wagonjwa 44,714 waliogunduliwa mwaka 2017., huku akisisitiza kuwa tatizo la ugonjwa wa Kifua Kikuu limeendelea kuwepo takribani mikoa yote nchini.
kwa upande mwingine, Waziri Ummya amesema kuwa, hadi kufikia Desemba 2018, jumla ya vituo vya kutolea huduma za Afya vilifikia 7,768 kutoka vituo 7,435 mwaka 2017 sawa na ongezeko la vituo 333 kwa mwaka, amedai kuwa Serikali ilikuwa inamiliki asilimia 71 ya vituo vya kutolea huduma; Mashirika ya dini asilimia 12, Taasisi za Serikali asilimia 3 na vituo binafisi asilimia 15.
Sambamba na hilo, waziri Ummy amesema kuwa, hadi kufikia Desemba mwaka 2018, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulikuwa na jumla ya wanachama 899,654 na ikihudumia jumla ya wanufaika 4,219,192 sawa na asilimia 8 ya Watanzania wote.
Social Plugin