Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATOA MSAMAHA KWA WAVUVU WASIO NA LESENI

Serikali imeagiza wavuvi waliokamatwa kwa kosa la kutohuisha leseni zao na vyombo vyao kwa mwaka 2019, waachiwe na makosa yao yafutwe mara moja.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alitoa agizo hilo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Ulega alisema wizara juzi ilipata taarifa kutoka vyombo vya habari kwamba wavuvi katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi hususani soko la Feri, Dar es Saalam, hawakwenda kuvua samaki kwa sababu ya kutokuwa na leseni za vyombo vyao na za uvuvi kwa mwaka 2019.

Kutokana na hali hiyo, Ulega aliagiza wavuvi wote waliokamatwa kwa kosa hilo kote nchini, kuachiwa mara moja kuendelea na shughuli zao.

Pia aliwataka maofisa uvuvi kutoka katika ofisi zao na kuwafuata katika mialo mbalimbali ili kuwakatia leseni.

"Kwa kuzingatia kuwa hiki ni kipindi cha mwanzo wa mwaka na leseni zinatolewa, wizara inaelekeza kwamba wavuvi wote waendelee kukatiwa leseni hadi Januari 31,” alisema Ulega.

Aidha, aliagiza maofisa wote wa wizara na halmashauri katika kipindi hiki wawafuate wavuvi kwenye mialo ili kuwakatia leseni wenye sifa kulingana na sheria na kanuni za uvuvi.

Aliongeza kuwa katika kutekeleza jukumu hilo wizara imekuwa ikiendesha operesheni dhidi ya uvuvi haramu na biashara haramu ya samaki na mazao yake kwa takribani mwaka mzima.

"Shughuli za uvuvi zinatakiwa kutekelezwa kwa mujibu wa sheria ya uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 pamoja na sheria nyingine za nchi. Kwa kuzingatia hilo, kila mtu anayehusika na uvuvi, anatakiwa kuwa na leseni halali ya uvuvi na leseni ya chombo anachotumia,” alisema Ulega.

Chanzo:Mpekuzi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com