Kutoka kushoto ni Rais wa TFF Wallace Karia, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson na Mfanyabishara Mohamed Dewji walipokuwa wakishangilia goli la tatu la Simba.
Simba SC imeanza vyema mechi zake za Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Jeunesse Sportive de la Saoura, ijulikanayo kama JS Saoura au JSS jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Nyota wa mchezo wa leo alikuwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi aliyefunga bao moja na kuseti mawili mawili mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa, Joshua Bondo aliyesaidiwa na washika vibendera Kitso Madondo Sibanda na Moemedi Monakwane wote wa Botswana, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji wake hodari, Okwi ‘Mtoa Roho’ dakika ya 45 na ushei kwa shuti kali baada ya ‘kuwapinduapindua’ mabeki wa JS Saoura kufuatia pasi ya kiungo Mzambia, Clatous Chama.
Okwi aliyekuwa katika kiwango cha juu leo, alifunga bao hilo akitoka kukosa bao la wazi baada ya kugongesha nguzo ya juu akiwa tayari amemtoka beki anatazamana na kipa.
Beki Mghana, Nicholas Gyan naye akapoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 33 baada ya kupiga nje akiwa ndani ya boksi na tayari amemuacha beki anatazamana na kipa.
Okwi ‘akawapinduapindua’ wachezaji wa JS Saoura tena dakika ya 35 na kupiga shuti kali kutoka umbali wa mita 27 lililopanguliwa na kipa Khaled Boukacem Hammar.
Simba SC ikapata pigo baada ya Nahodha wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ kuumia dakika ya 34 na kutolewa nje kwa machela kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji mwenzake, Meddie Ksgere kutoka Rwanda.
Mabadiliko hayo ya dharula yakaiongezea makali safu ya ushambuliaji ya Simba hadi kupata bao lao. Kwa ujumla, JS Saoura hawakuwa na madhara kipindi cha kwanza kutokana na kucheza kwa kujihami na kushambulia kwa kushitukiza.
Refa wa akiba Oamogetse Godisamang wa Botswana mwishoni mwa kipindi cha kwanza alimfuata kocha wa Simba SC, Mbelgiji Patrick Aussems kwenda kumkumbusha kutulia katika eneo lake baada ya kuanza kumuona anaingiwa na kimuhemuhe cha mchezo.
Kipindi cha pili, Simba SC walirudi na nguvu mpya na kufanikiwa kupata mabao mawili zaidi yote yakifungwa na mtokea benchi, Kagere Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda na mar azote akimalizia kazi nzuri ya Okwi.
Kagere alifunga bao la pili dakika ya 51 akimalizia pasi ya Okwi ambaye mabeki wa JS Saoura walimuacha wakidhani ameotea baada ya pasi ndefu ya Chama Kagere tena akafunga dakika ya 67 kwa mara nyingine akimalizia pasi nzuri ya Okwi, akaingia nayo ndani kidogo kabla ya kumtungua kipa Khaled Boukacem kwa mpira wa juu.
Bao hilo liliwavunja kabisa nguvu JS Saoura ambao kipindi cha pili walimuingiza mshambuliaji wao mpya, Mtanzania Thomas Emmanuel Ulimwengu.
Safu ya ulinzi ya Simba SC leo ilicheza vizuri chini ya Muivory Coast, Serge Wawa Pascal na Mganda Juuko Murshid ambaye leo anacheza kwa mara a kwanza baada ya muda mrefu kufuatia mzawa, Erasto Nyoni kuumia.
Mechi ya Kundi D inafuatia Saa 4:00 usiku wa leo Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria kati ya wenyeji, Al Ahly dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Baada ya mchezo wa leo, Simba SC itasafiri kuwafuata AS Vita mjini Kinshasa Januari 19, wakati JS Saoura watakuwa wenyeji wa Ahly Januari 18 nchini Algeria.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Pascal Wawa, James Kotei, Hassan Dilunga/Muzamil Yassin dk65, Jonas Mkude, John Bocco/Meddie Kagere dk37, Emmanuel Okwi/Shiza Kichuya dk86 na Clatous Chama.
JS Saoura; Khaled Boukacem, Hamza Zaid/Aimen Abdelaziz Lahmeri dk62, Ziri Hammar, Ibrahim Beckakchi, Naceredine Khoualed/ Mohamed El Hadi Boulaouidet dk74, Younes Koulkheir/Thomas Ulimwengu dk55, Messala Merbah, Fateh Talah, Emad Eddine, Mohamed Hammia na Ibrahim Farhi.
Social Plugin