Wanaowania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika
Tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika inatarajiwa kutolewa leo Jijini Dakar nchini Senegal, ambapo jumla ya mastaa watatu wanaocheza Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Mohamed Salah, Pierre-Merick Aubameyang na Sadio Mane.
Listi hiyo ni marudio ya wachezaji watatu waliotajwa kuwania tuzo ya msimu uliopita, ambapo itatolewa kwa kuzingatia kiwango cha mchezaji husika katika mwaka 2018.
Pierre-Merick Aubameyang ambaye ni raia wa Gabon, amefanikiwa kuwepo katika listi ya mwisho ya wachezaji watatu wa tuzo hizo kwa mara ya tano mfululizo sasa tangu mwaka 2014 na kuifikia rekodi ya mkongwe wa Ivory Coast, Yaya Toure na wa Ghana, Michael Essien.
Mohamed Salah ambaye aliweka historia ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Misri kushinda tuzo hiyo tangu ilipoasisiwa mwaka 1992. Ametajwa katika listi ya wachezaji watatu wa mwisho kwa miaka miwili mfululizo huku akishinda kwa mara ya kwanza msimu uliopita.
Kwa upande wa Sadio Mane, ametajwa katika listi ya wachezaji watatu wa mwisho wa tuzo hiyo kwa mwaka wa tatu mfululizo huku akiwa hajashinda tuzo hiyo mpaka sasa.
Jana, Januari 7, ulifanyika mchezo wa mastaa wa zamani wa soka barani Afrika, mchezo uliohusisha kati ya magwiji wa soka wa Senegal walioshiriki katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002 na magwiji wa zamani wa soka kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika, akiwemo mchezaji bora wa Dunia na Rais wa Liberia, George Weah.
Pia kabla ya kilele cha tuzo hizo, Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF itafanya kikaom maalum ambacho kitatangaza nchi itakayoandaa michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu, baada ya nchi ya Cameroon kupokonywa uenyeji wa michuano hiyo kwasababu ya kutokidhi vigezo.
Social Plugin