Katika mchezo wa soka timu kufunga mabao ni jambo muhimu zaidi. Ukifanya hivyo ndio unashinda. Bila shaka kwamba kama unataka kuwa na uhakika wa kushinda kwenye kila mchezo wa soka, ukifunga mabao mengi zaidi ndiyo yanayokuwezesha kukufanya uwe mshindi.
Baada ya Manchester City kuonyesha kiwango cha juu na kufunga mabao 9-0 dhidi ya Burton Albion kwenye mchezo wa Carabao, hapa tunakuchambulia timu zilizowahi kupata ushindi mkubwa zaidi katika historia ya mchezo wa soka nchini England.
9. Manchester United 9-0 Ipswich (Machi 4, 1995)
Mashetani Wekundi hao waliibuka na ushindi wa mabao 9-0 dhidi ya Ipswich na hadi sasa imebakia kuwa rekodi kwenye zama za Ligi Kuu ya England.
Andy Cole alifunga mabao matano – akiweka rekodi ya kufunga mabao mengi kwenye mchezo mmoja wa Ligi Kuu, huku Roy Keane akifunga, Mark Hughes (mawili) pamoja na Paul Ince akifunga moja.
Kichapo hicho kilikuwa cha kushangaza kwa kuwa Ipswich iliichapa United 3-2 kwenye mchezo wa mwanzoni mwa msimu huo.
8. West Ham United 10-0 Bury (Oktoba 25, 1983)
Ushindi mwingine wa kushangaza ni kwenye mchezo wa Kombe la Ligi, wagonga nyundo hawa wa London walipata ushindi mkubwa zaidi katika historia yao.
Tony Cottee ambaye alikuwa na umri wa miaka 19 peke yake alitikisa nyavu mara nne, huku Trevor Brooking aliyekuwa na miaka 36 alifunga mawili dhidi ya Bury, ambao walikuwa vinara wa ligi daraja la kwanza na walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo.
7. Liverpool 10-0 Fulham (Septemba 23, 1986)
Huu ulikuwa ni mchezo wa Kombe la Ligi na wekundu hawa wa Anfield walitoa kichapo cha kihistoria.
Uwanja ukiwa na watazamaji 13,498 pale Anfield ulishuhudia Steve McMahon na Ian Rush wakiiangamiza Fulham. McMahon alifunga mabao manne, lakini alikosa penalti kwenye mchezo huo. Liverpool walitinga fainali ya Kombe la Ligi lakini wakaja kufungwa na Arsenal magoli 2-1.
6. West Brom 12-0 Darwen (Aprili 4, 1982)
Darwen FC ilikuwa ni timu kutoka pale mitaa ya Lancashire, ambayo ilionekana kuwa na matarajio makubwa kwenye soka la England.
Lakini walipokutana na West Brom kwenye Ligi Daraja la Kwanza wakajikuta wakikumbana na kipigo cha mabao 12-0.
5. Nottingham Forest 12-0 Leicester City (Aprili 21, 1909)
Nottingham Forest ilikuwa ni timu tishio wakati huo na walipokutana na Leicester waliitandika bila huruma mabao 12. Gwiji wa Forest na ambaye ndiye mfungaji wa wakati wote wa timu hiyo, Grenville Morris, alifunga mabao mawili kwenye mchezo huo.
4. Newcastle United 13-0 Newport County (Oktoba 5, 1946)
Wakati huo wakiwa wanacheza Ligi Daraja la pili, Newcastle walitoa kipigo cha aina yake, huku kipindi cha kwanza wakiongoza kwa mabao saba.
Mchezaji, Len Shackleton ambaye ndio alikuwa ametoka tu kujiunga na klabu hiyo kwa ada ya pauni 13,000, alifunga mabao sita peke yake na kuwafanya vijana hao kuondoka uwanjani wakiwa na shangwe kubwa.
3. Stockport County 13-0 Halifax Town (Januari 6, 1934)
Miaka 85 iliyopita Stockport waliweka historia kwenye soka la England ambao hawajawahi kuifikia tena hadi leo.
Stan Milton alikuwa akicheza mchezo wake wa kwanza kwenye Ligi Daraja la Tatu na hadi kipindi cha kwanza kinamalizika ubao ulikuwa unasomekana 2-0 Stockport wakiwa wanaongoza. Lakini kipindi cha pili Milton alifunga mabao 11 peke yake na kuweka historia yake kwenye mchezo huo hadi leo.
2. Clapton 0-14 Nottingham Forest (Januari 17 January 1891)
Forest waliweka tena historia nyingine. Huu ulikuwa mchezo wa raundi ya nne ya Kombe la FA wakaifunga Clapton mabao 14-0 na kujiandikia historia yao.
1. Preston North End 26-0 Hyde FC (Oktoba 15, 1887)
Hii ndio historia iliyoshindwa kuvunjwa hadi leo kwenye soka huko England na itachukua miaka mingi kuweza kuivunja.
Ni miaka 131 iliyopita, Preston wakiwa kwenye dimba la nyumbani waliifumua Hyde FC mabao 26-0 kwenye uwanja wa Deepdale ukiwa ni mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la FA.
North End kwenye mchezo huo iliweka rekodi ya aina yake katika historia ya soka la Uingereza: Kufunga mabao mengi kwenye mchezo mmoja, kupata ushindi mkubwa zaidi nyumbani ambao ni rekodi hadi leo.
Cha kuchangaza licha ya ushindi huo mnono na kuweza kutinga fainali, lakini wakaja kufungwa na West Brom 2-1.
Social Plugin