Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWALIMU ATEKWA,ANYWESHWA SUMU NA KUFARIKI AKIJIANDAA KUOA

Mwalimu Nocka Mwaisango (28) wa Shule ya Sekondari Kibwe, jijini Dodoma, amefariki dunia baada ya kunyweshwa sumu na watu wasiofahamika.

Alikufa wakati akitokea mkoani Dodoma kwenda kijijini kwao mtaa wa Mtakuja, Mbalizi Wilaya ya Mbeya Vijijini kwa lengo la kumuoa mchumba wake wa muda mrefu.

Baba mzazi wa mwalimu huyo, Oddy Mwaisango, alisema alipigiwa simu Desemba 20, mwaka jana na mtoto wake huyo kuwa anatarajia kwenda Mbeya kwa mapumziko ya sikukuu na kwamba atatumia mapumziko hayo kumuoa mchumba wake wa muda mrefu.

Alisema baada ya kupigwa simu hiyo, alishangaa kuona muda mrefu unapita bila kumuona na wiki moja baadaye alipigiwa simu na watu wasiofahamika waliotumia namba ya simu ya mtoto wake wakisema kuwa wanamshikilia kwa kazi maalum.

Alisema baada ya kauli hiyo aliamua kwenda Kituo cha Polisi Mbalizi, kuripoti tukio hilo.

Alisema siku iliyofuata mama yake alienda Dodoma katika shule aliyokuwa akifundisha kukutana na Mwalimu Mkuu ambaye alimjibu kuwa mtoto wake hakumuaga alipoondoka.

Alisema, ilibidi aende kuripoti Polisi Dodoma na Kitengo cha Uchunguzi wa Mawasiliano mkoani humo kiligundua kuwa mwalimu huyo yuko mkoani Morogoro.

“Ilibidi mama yake asafiri hadi Morogoro na aliripoti kituo cha polisi na kukabidhiwa mtu wa uchunguzi wa mitandao ndipo katika kuchunguza wakabaini wahalifu hao na mwalimu huyo wako mkoani humo, lakini ghafla wakawa hawaonekani kwenye mtandao,” alisimulia.

Alisema baadaye wahalifu hao walimpigia simu (baba) wakihitaji Sh. 5,000,000 kama kikombozi, lakini kwa sababu hakuwa na fedha aliwatumia Sh. 500,000 ili wamwachie.

Aliongeza kuwa siku iliyofuata mtoto wake aliwapigia simu mwenyewe na kuwaambia kuwa yuko kituo cha daladala cha Tazara Mbeya na walipoenda kumfuata walikuta hajitambui.

Aidha, alisema waliamua kumkimbiza hospitali ya Ifisi iliyoko Wilaya ya Mbalizi na baadaye walimhamishia Hospitali ya Rufani Mbeya.

Alisema akiwa wodini aliongezewa maji ya kutosha, lakini alikuwa analalamika kuumizwa kwenye koo na kifuani na katika uchunguzi wa madaktari ilibainika amenyweshwa sumu.

Alisema siku iliyofuata mwalimu huyo alifariki akiwa hajawataja waliomfanyia unyama huo huku chanzo cha kifo kikitajwa kuwa ni dawa aina ya ‘Asphxia Due Mothorax’ aliyonyweshwa.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kibwe, Dodoma, Mwasiti Msokola, alikiri kupata taarifa za kifo cha mwalimu wake na kwamba suala hilo linashughulikiwa na mkurugenzi ambaye ndiye mwajiri wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Chanzo:Nipashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com