Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka,akizungumza na Wahadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe waliohudhuria warsha ya mabadiliko katika Sekta ya ajira kwa manufaa ya Jamii Afrika Mashariki (TESCEA) inayoendelea Morogoro.
Mwezeshaji wa warsha hiyo kutoka nchini Kenya Prof. Charles Kingsburry akifafanua kuhusu mradi huo kwa Waandishi wa Habari.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe (Taaluma) Prof. Ganka Nyamsogoro akiwasisitiza washiriki umuhimu wa warsha hiyo katika kubadili mbinu za ufundishaji.
Baadhi ya washiriki wakiwa katika majadiliano.
Mratibu wa mradi wa TESCEA Dkt. Albogast Musabila akifafanua kuhusu mradi huo kwa Waandishi wa Habari.
Mwezeshaji toka Chuo Kikuu, Afrika Nazarene cha nchini Kenya Dkt. Kendi Muchungi akieleza umuhimu wa mpango huo na jinsi unavyoweza kunufaisha wasomi na Jamii zao.
Mratibu Msaidizi wa mradi wa TESCEA wa Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Jennifer Sesabo akitambulisha mpango wa mradi huo kwa Washiriki.
Washiriki wakifuatilia maelekezo yanayotolewa katika warsha hiyo inayoendelea Hoteli ya Morogoro.
Washiriki wa warsha ya TESCEA katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi rasmi.
***
Chuo Kikuu Mzumbe kupitia mradi wake mpya wa ‘TESCEA’ kimeendesha warsha ya kuwajengea uwezo wahadhiri katika mbinu bora za ufundishaji zinazosaidia wanafunzi kuweza kujiajirika pindi wanapohitimu masomo yao ya elimu ya juu.
Akizungumza katika uzinduzi wa warsha hiyo inayoendelea katika hoteli ya Morogoro, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka amesema Chuo Kikuu Mzumbe ni mahiri katika kufundisha masomo ya biashara na menejimenti na sasa kinakwenda hatua ya mbele zaidi kwakuwaandaa wahitimu wa ndani na hata nchi nyingine kutengeneza ajira kabla ya kuhitimu masomo yao.
Prof.Kusiluka ameeleza kuwa kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa waajiri dhidi ya wahitimu wa vyuo vikuu nchini na kuonekana kutokuwa na ujuzi wa kutosha na umahiri katika fani walizosomea pindi wanapotaka kuajiriwa.
Hivyo, Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma na vyuo vikuu viwili kutoka Uganda (Uganda Martys na Gulu), pamoja na asasi za AFELT, LIWA, ASHOKA kutoka Kenya na INASP kutoka Uingereza, wameanza kwa kuwajengea wahadhiri ili kubadili mbinu za ufundishaji zitakazowawezesha wahitimu kuwa na maarifa, ubunifu na ujuzi zaidi kutambua na kutumia fursa zilizopo ili kutengeneza ajira au kuajiriwa.
Kwa upande wake mwezeshaji wa warsha wa asasi ya umoja wa Vyuo vikuu vinavyofundisha mbinu zinazohitajika katika kuboresha ufundishaji Afrika Mashariki (AFELT) na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Daystar cha Kenya Prof.
Charles Kingsburry, amesema ni muhimu sasa kubadili mfumo wa ufundishaji unaowafanya wahitimu kujua vitu kulingana na elimu wanayofundishwa darasani pekee na kwa kutegemea mitandao ya intaneti na badala yake mbinu mpya za ufundishaji ziwajenge katika ubunifu ,maarifa,mbinu na stadi halisia zitakazowawezesha kujiajiri wao na kuweza kuajiri watu wengine.
Hii ina lengo si tu la kuwafanya wahitimu kujua vitu tofauti bali kuwajenga kuwa watu tofauti wanaoleta mabadiliko chanya kwa jamii nzima na kujinufaisha wao na jamii zinawazunguka kupitia elimu waliyopata.
Naye mwezeshaji mwingine kutoka Asasi ya AFELT na mhadhiri wa Chuo Kikuu, Afrika Nazarene cha nchini Kenya Dkt. Kendi Muchungi amesema wahitimu wa Vyuo Vikuu vyote vya Afrika Mashariki hawatofautiani na wamekuwa wakikosa uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa na hivyo kushindwa kuisaidia jamii katika suala la ajira kupitia elimu waliyopata,badala yake wamekuwa wakitegemea kuajiriwa. Hivyo ni imani yake kuwa mpango huo utaleta mabadiliko kwa wahadhiri wa vyuo vikuu katika ufundishaji na kunufaisha jamii nzima ya Afrika Mashariki kupitia wasomi wachache.
Wakati huo huo mratibu wa Mradi wa ‘TESCEA’ kutoka Chuo Kikuu Mzumbe,Dkt.Albogast Musabila amesema pamoja na lengo kuu la mpango wa mradi huo la kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri na kuajiri,Chuo Kikuu Mzumbe kwa ushirikiano na wadau wa Sekta ya ajira, wahadhiri na wanafunzi kimeanza mchakato wa kukusanya maoni ya wadau kwa ajili ya kuandaa mapendekezo yatakayozingatiwa wakati wa kuboresha mitaala na kuanzisha mitaala mipya.
Social Plugin