TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KULAANI MAUAJI YA WATOTO WASIOKUWA NA HATIA MKOANI NJOMBE
1.0 Utangulizi
Sisi waanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) Kanda ya Ziwa tumesikitishwa sana na mauaji ya watoto kumi (10) yaliyotokea Mkoani Njombe (Nyanda za juu Kusini) na kuacha simanzi kubwa kwa Taifa, familia, ndugu jamaa na marafiki. Hivyo basi tunaungana na wapenda amani wote nchini kwenye kuomboleza msiba huu wa kitaifa.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la polisi na waandishi mbali mbali ambao wamekuwa wakifwatilia suala la mauaji ya watoto hao, chanzo kikubwa cha mauaji hayo ni imani za kishirikina. Watu (waganga) ambao wamekuwa wakihusishwa na imani za kishirikina wamekuwa ni chanzo cha mauaji yaliyotokea mjini Njombe. Waganga hao wamekuwa wakiua wakiteka watoto na kuwaua huku wakichukua sehemu mbali mbali za miili yao. Aidha, jeshi la polisi linaendelea na upelelezi kuhakikisha wauaji hao wanatiwa nguvuni na kujibu mashtaka yatakayowakabili.
Ndugu Waandishi wa habari ifahamike kuwa haki ya kuishi ni haki ya msingi na ya Kikatiba kwa kila binadamu. Nchini Tanzania haki hiyo inalindwa na Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) kupitia Ibara ya 14. HIvyo basi kuvunja haki hii ni kukiuka Katiba pamoja na mikataba mbali mbali ya Kimataifa ambayo Tanzania ni nchi mwanachama.
Ndugu waandishi, mauaji yaliyotokea Mkoani Njombe siyo ya kufumbiwa macho kwani kitendo hicho ni uhalifu mkubwa unaokiuka msingi wa haki ya kuishi na utu wa binadamu. Katika taifa letu hakuna mwenye mamlaka ya kuiondoa roho ya binadamu mwingine isipokuwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Hata hivyo, historia yetu kama taifa la Tanzania japo bado tuna sheria inayomruhusu Rais kusaini adhabu ya kifo, ni mara chache sana tumeshuhudia marais wetu wastaafu na rais aliyepo madarakani wakisaini adhabu hii ya kifo. Ni dhahiri kwamba, suala la kutoa uhai wa mtu ni jambo baya kutokea katika taifa letu.
2.0 Ulinzi wa Mtoto Kisheria
Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 kifungu cha 9 inasema; mtoto ana haki ya KUISHI kujaliwa utu wake, kuheshimiwa, kupumzika (kucheza), kuwa huru, kuwa na afya bora, kupata elimu pamoja na makazi kutoka kwa wazazi wake.
Hata hivyo, jukumu hili la ulinzi wa maisha ya mtoto lipo pia Kikatiba na katika Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kila mtu ana wajibu wa kulinda na kuteteta Katiba na sheria za nchi.
Ipo pia mikataba ya Kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama ambayo imeweka haki mbali mbali za mtoto ikiwemo haki ya kuishi. Baadhi ya Mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa kuhusu watoto wa mwaka 1989, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kisiasa na Haki za Kiraia wa mwaka 1966, Nyongeza ya Mkataba wa Maputo wa Mwaka 2003.
Mikataba yote hii na mingine inaelekeza juu ya haki za watoto na ulinzi wa utu wao.
Ndugu waandishi mauaji ya watoto kumi ni ukatili mkubwa, kwani uhai wa watoto hawa umekatisha ghafla maisha na ndoto zao na kuleta simanzi kubwa kwa ndugu jamaa , marafiki na taifa kwa ujumla. Taifa limepoteza kizazi ambacho kingeweza kulitumikia kwa maslahi mapana ya nchi.
Ndugu waandishi wa habari, Ikumbukwe kuwa watoto ni kundi ambalo kwa namna moja ama nyingine hawawezi kupata haki zao bila ya msaada wa watu wengine. Hivyo basi, inapotokea kundi hili la watoto linaathirika na matendo ya kinyama kama haya ya mauaji, ni jukumu letu sote kukemea vikali na kupaza sauti zetu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wauaji wa watoto hawa.
Hivyo basi, nyinyi kama waandishi wa habari na sisi watetezi wa haki za binadamu naomba tushikamane katika kipindi hiki kuwasemea watoto na kuhakikisha haki na utu wao unalindwa wakati wote.
3.0 Wito Wetu
Jeshi la polisi lifanye uchunguzi wa kina na kuwabaini wote waliohusika na mauaji tajwa na kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wote waliohusika na mauaji hayo.
Vyombo vya ulinzi na usalama viwe macho na waganga wanaohusisha utajiri/mafanikio na vitendo vya kishirikina na kuwachukulia hatua stahiki pindi wanapokiuka sheria na Katiba ya nchi.
Waandishi wa habari watumie kalamu zao kwenye kutoa elimu kwa jamii juu ya athari za ushirikina ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa kero kwa jamii na kusababisha hasara na simanzi kwa ndugu, jamaa, marafiki na taifa kwa ujumla.
Jamii ishiriki kikamilifu kwenye kuripoti viashiria vya ushirikina na uvunjifu wa haki za binadamu katika jamii.
Tamko hili limetolewa na wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu kanda ya Ziwa.
Mashirika Wanachama
OJADACT
ADLG
WOTE SAWA
SAUTI YA WANAWAKE UKEREWE
UVUUMA
Na Edwin Soko
Social Plugin