Jeshi la Polisi mkoani Songwe limemfikisha mahakamani dereva Mawazo Jairos (29) kwa kosa la kupigana na askari watatu wa Kikosi cha Usalama Barabarani.
Licha ya dereva huyo kufikishwa mahakamani, amelalamikia kitendo cha kung’atwa eneo la shingoni na mgongoni na mmoja wa askari wakati wakipambana naye kwa madai alishindwa kutii amri bila shuruti.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Yusuf Sarungi jana alisema tukio la dereva na askari hao lilitokea Januari 12, mwaka huu saa 2:30 asubuhi Mtaa wa Transfoma mjini Tunduma.
Kamanda Sarungi alisema mtuhumiwa alifikishwa mahakamani na kusomewa shtaka la kuzuia askari kufanya kazi yao na shambulio la kudhuru mwili.
Alidai siku ya tukio, askari hao walikuwa na maofisa wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) ambao walikuwa na operesheni ya ukaguzi wa magari.
Kamanda Sarungi alidai katika ukaguzi huo walisimamisha gari lenye namba za usajili T 842 AAC aina ya Mistubishi Fuso, likiendeshwa na Jairos mkazi wa Mbeya.
Alisema baada ya kusimamishwa Jairos anadaiwa kutoa lugha chafu za kashfa na matusi kwa askari na maofisa wa Sumatra.
Alidai kuwa dereva huyo akiwa kwenye njia ya vumbi kutoka eneo la Mwaka kwenda Songea, aliondoa gari hilo bila kuruhusiwa kitendo kilichowalazimu maofisa hao kulikimbiza na walipofika eneo la Makambini walifanikiwa kumkamata.
Kamanda Sarungi alidai kuwa baada ya gari hilo kukamatwa, Jairos alishuka akiwa amehamaki na kuanza kutoa lugha za matusi kwa maofisa.
Alidai kuwa dereva huyo ghafla alianza kuwashambulia askari, lakini wakafanikiwa kumdhibiti.
Kamanda Sarungi alidai kuwa dereva huyo alianza kupiga kelele kuwa askari hao wanamuua na wananchi wakajaa na kuwazuia askari wasiendele kumpiga.
Alidai kuwa baada ya askari hao kumwachia, alipata upenyo na kuingia katika gari, kisha kutoka na panga akaanza kuwatishia baadaye alifanikiwa kuondoka na gari hilo kabla ya kukamatwa katika mji wa Vwawa wilayani Mbozi.
Social Plugin