Tundu Lissu amehitimisha matibabu yaliyomchukua siku 480 baada ya kuondolewa vyuma vilivyokuwa katika mguu wake wa kulia ambavyo aliwekewa Julai 9, mwaka jana ili kuunganisha mifupa.
Baada ya kuhitimisha matibabu hayo yaliyotokana na majeraha aliyopata baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana mwaka juzi, mbunge huyo wa Singida Mashariki, amesema anatarajia kutoa waraka alioeleza umebeba ujumbe mzito juu ya masuala mbalimbali likiwamo tukio hilo na hali ya kisiasa nchini.
Akizungumza na Mwananchi jana, Lissu alisema alifanyiwa upasuaji wa mwisho wa kuondoa vyuma hivyo Jumatatu iliyopita mchana.
“(Upasuaji) ulichukua kama saa moja na nusu. Niliingia chumba cha upasuaji saa 6:30 mchana na nikatoka huko saa nane mchana.Baada ya hapo nilipelekwa chumba cha mapumziko kwa saa mbili za uangalizi halafu nikarudishwa chumbani kwangu saa 10:30 jioni.”
Lissu alishambuliwa mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake Area D, mjini Dodoma wakati akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge. Alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya.
Alipata matibabu katika hospitali hiyo hadi Januari 6, mwaka jana alipohamishiwa Ubelgiji.
Hivyo, tangu Septemba 7, 2017 hadi Desemba 31, 2018, mwanasheria huyo mkuu wa Chadema ametibiwa kwa kipindi cha siku 480 sawa na mwaka mmoja, miezi mitatu na siku 24.
Via Mwananchi
Social Plugin