Mwanamke mmoja nchini Uingereza amepata majeraha ya kemikali baada ya kupewa kwa makosa dawa ya kusimamisha uume badala ya dawa ya kutibu macho.
Mwanamke huyo kutoka Glasgow, Uskochi alipewa dawa ya kupaka ya Vitaros badala ya VitA-POS.
Daktari wake alimuandikia dawa sahihi ya kutibu matatizo ya macho ya VitA-POS, ambayo ipo katika mfumo wa kiminika kilaini.
Hata hivyo, kulitokea mkanganyiko wa kusoma maandishi ya daktari na mfamasia akatoa dawa ya Vitaros, ambayo pia ipo katika mfumo wa kiminika laini, lakini yenyewe huchochea kusimama kwa uume.
Baada ya kupaka dawa hiyo, alipata maumivu makali, jicho kuvimba hali iliyompelekea kushindwa kuona vizuri.
Majeraha hayo ya kemikali hata hivyo yaliweza kutibika, na jicho lake kusafishika baada ya siku chache.
Mkasa wa mwanamke huyo umeandikwa kwenye jarida la BMJ Case Reports. Jarida hilo limewataka madaktari kutumia herufi kubwa ili kuepuka makosa kama hayo kutokea.
Maandishi yalofanana
Daktari Magdalena Edington, ambaye ameandika ripoti hiyo amesema: "Makosa katika kutoa dawa ni jambo la kawaida. Dawa zenye vifungashio na majina yafananayo zinaongeza hatari za kutokea makosa hayo.
"Hata hivyo, ni jambo la kustaajabisha katika mkasa huu kuwa hakuna hata mtu mmoja, akiwemo mgonjwa mwenyewe, daktari na mfamasia ambaye alijiuliza iweje mgonjwa mwanamke apewe dawa ya matatizo ya kiume.
"Tunaamini kuwa mkasa huu ni muhimu sana kuuripoti ili kukuza uelewa wa kutoa dawa kwa njia salama."
Social Plugin