Marekani imeliwekea vikwazo shirika la mafuta la serikali ya Venezuela PDVSA na kulitaka jeshi la nchi hiyo kuyaunga mkono mabadiliko ya amani ya uongozi.
Mshauri wa masuala ya ulinzi wa rais Donald Trump John Bolton amedai kuwa rais wa Venezuela Nicolás Maduro na washirika wake hawataweza tena kuiba rasilimali za raia wa Venezuela.
Harakati za upinzani nchini humo kuung'oa madarakani utawala wa Maduro zimeshika kasi katika kipindi cha siku za hivi karibuni.
Marekani na nchi zaidi ya 20 zinamtambua kiongozi wa upinzani Juan Guaidó kama rais wa mpito wa nchi hiyo.
Waziri wa Fedha wa Marekani Steven Mnuchin amesema mapato yatakayotokana na uuzwaji wa mafuta kutoka nchi hiyo yatazuiwa kwenda kwenye mifuko ya serikali ya Maduro.
Kampuni hiyo inaweza kuondokana na vikwazo pale itakapomtambua Guaidó kama rais halali.
Chanzo:Bbc
Social Plugin