Kamati ya maandalizi ya michuano ya Mapinduzi mwaka 2019, inayofikia tamati leo, imeeleza kuwa timu za Azam FC na Simba zimesafiri leo kwa ndege kutoka Unguja kwenda Pemba tayari kwa mchezo wa fainali.
Kamati hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wake imeeleza kuwa timu hizo ambazo zimecheza mechi za makundi na nusu fainali katika visiwa vya Unguja imebidi zisafiri kwa ndege ya kukodi ili kwenda kumaliza fainali leo.
''Maandalizi yote kwaajili ya mchezo wa fainali yamekamilika na timu zimesafiri kwa ndege leo, hivyo mchezo utafanyika muda uliopangwa kwenye uwanja wa Gombani ambao una ubora wa kutosha'', amesema.
Azam FC inacheza fainali yake ya tatu mfululizo huku ikiwa tayari imeshachukua ubingwa huo katika fainali zote mbili zilizopita ikiwemo ile ya mwaka jana (2018) ambayo waliwafunga Simba.
Kwa upande wa Simba wachezaji Haruna Niyonzima, Shiza Kichuya na Rashid Juma tayari wamewasili visiwani Pemba kuongeza nguvu kwenye kikosi cha Simba ambacho kina wachezaji wengi wa kikosi B.
Social Plugin