Uamuzi wa mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kuwaondoa ukumbini mkurugenzi na mwenyekiti wa halmashauri ya Hai waliokuwa wakiongoza kikao cha kamati ya fedha umezua taharuki kwa viongozi hao.
Mkurugenzi huyo, Yohana Sintoo na mwenyekiti, Helga Mchomvu na wajumbe wengine waliondolewa katika ukumbi huo huku mkuu huyo wa wilaya akiingia na watu wengine kwa ajili ya kutumia ukumbi huo.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi leo jioni Jumanne Januari 15, 2019, Sabaya amesema aliwaondoa akiwataka kutumia ukumbi mwingine.
Amesema kikao hicho kilikuwa na wajumbe 10, aliwataka kuhamia ukumbi mdogo ili yeye ahudumie zaidi ya wamachinga 200 walioomba ukumbi huo mkubwa mapema.
Akisimulia tukio hilo leo, Mchomvu amesema kitendo hicho hakipaswi kufanywa na kiongozi huyo wa Serikali.
“Tulikuwa na kikao cha kamati ya fedha katika ukumbi wa Halmashauri. Tumeanza tangu saa 4 asubuhi hadi saa 6 mchana. Aliingia mkuu wa wilaya na kututaka kutoka nje ya ukumbi na kuamuru waliokuwa naye nje ya ukumbi huo, kuingia ndani,” amesema.
Na Janeth Joseph, Mwananchi
Social Plugin