Waziri wa Elimu Prof. Joyce Ndalichako
Tatizo la ucheleweshaji wa fomu kwa wazazi za kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu limechangia idadi kubwa ya wanafunzi kushindwa kuripoti kwa wakati shuleni kujiunga na masomo yao.
Hali hiyo ilielezwa jana na wazazi wa wanafunzi hao akiwemo Diwani wa Kata ya Busoka katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, mkoani Shinyanga Julius Malale,ambaye alisema hali ya kuchelewa kupata kwa muda fomu hizo kumechangia wazazi kushindwa kufanya maandalizi mapema ya watoto wao.
Katika Shule ya Sekondari Nyandekwa juzi,ikiwa siku ya kwanza ya kufungua shule hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyeripoti kuanza shule,kitendo ambacho kinaelezwa kuwa cha kwanza shuleni hapo kutokea tangu kuanzishwa kwa shule hiyo.
Hata hivyo kwa mujibu wa Kaimu Ofisa Elimu ya Sekondari katika Halmashauri ya Mji wa Kahama,Neema Lema,alisema hadi jana siku ya Jumanne ni wanafunzi watatu tu ndiyo walioripoti katika shule hiyo ya Sekondari Nyandekwa,ingawa alidai tatizo halikuwa lao bali lilikuwa upande wa wazazi.
Neema alisema hali hiyo imejitokeza kutokana na wazazi wa wanafunzi wanaostahili kuanza kidato cha kwanza,kutozifuata mapema fomu hizo kwenye shule za msingi pale watoto wao walikuwa wakisomea.
Alisema ofisi yake ilirahisisha upatikanaji wa fomu hizo kwa kuzipeleka katika shule za msingi walizosomea wanafunzi hao mapema ,lakini wazazi wenyewe wameshindwa kuzichukua kwa wakati ili vijana wao wahudhurie masomo kwa wakati.
Pamoja na hayo baadhi ya wadau wa elimu mjini Kahama,akiwemo Juma Mapolu,walisema ukata mkubwa wa fedha kwa wazazi ni sababu kubwa iliyochangia hali hiyo.
Mapolu alisema pamoja na elimu bure lakini hiyo haisadii sana kwa wazazi kuwakuwa gharama za maandalizi ili mtoto aweze kuanza kidato cha kwanza ni kubwa zaidi ya ada iliyofutwa ambayo ni Shilingi Elfu Ishirini kwa mwaka wakati maandalizi ni zaidi ya laki mbili.
Na Mwandishi wa Malunde1 blog - Kahama
Social Plugin