Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO MAZITO KWA MAAFISA USTAWI WA JAMII

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa watekeleze majukumu yao kwa bidii, weledi, uadilifu na wasijihusishe na vitendo vya rushwa.


Amesema maafisa hao wanatakiwa watumie mbinu shirikishi ambazo zinahusisha jamii yenyewe na wataalamu ambao ni watoa huduma ngazi ya jamii (Community Case Worker) ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.


Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo jana (Jumanne, Januari 29, 2019) kwenye Mkutano wa Mwaka wa Kiutendaji wa Maafisa Ustawi wa Jamii katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, jijini Dodoma.


Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka maafisa hao wahakikishe kwamba haki za msingi za makundi hayo zinapatikana kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo katika kutoa huduma ya taaluma yao.


Amesema taaluma ya Ustawi wa Jamii imepewa dhamana ya kuwa mlinzi wa mtoto, kumhudumia na kusimamia haki zake, hivyo amewatakawazuie na watokomeze aina zote za ukatili kwa watoto, wazee na wenye ulemavu.


Waziri Mkuu amesema jukumu hilo pia linahusisha watoto waliopo kwenye mazingira hatarishi na wanaoishi na kufanya kazi mitaani, wazee, wanawake wasio na uwezo na watu wenye ulemavu.


Amesema pamoja na mafanikio makubwa ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeyapata ni muhimu wakaendelea kuongeza nguvu na weledi ili kutorudi nyuma katika kujenga msingi wa kuimarisha ustawi wa makundi maalumu.


Pia, Waziri Mkuu amewaagiza maafisa hao wakasimamie utekelezaji wa mkakati wa Mkono kwa Mkono, Familia kwa Familia, Kaya kwa Kaya kupitia huduma ya kuzuia ukatili ngazi ya familia wenye lengo la kuzuia ukatili ndani ya familia ili ulete matokeo tarajiwa.


“Tambueni umuhimu wenu na kwamba jamii inawategemea kutekeleza majukumu yenu kikamilifu ili kupunguza matatizo ya kijamii kwa wale wenye uhitaji wakiwemo watoto, watu wenye ulemavu, wazee, familia zenye migogoro na akina mama wanaonyanyaswa na makundi mengine.”


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewashukuru wadau wa maendeleo kwa namna wanavyoshirikiana na Serikali katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo likiwemo suala la uimarishaji wa huduma za ustawi wa jamii nchini.


Amesema anatambua mchango mkubwa kutoka kwa shirika la UNICEF, USAID, UN WOMEN, UNFPA, John Snow Inc, Pact, HelpAge International, World Vision, Save the Children, Plan International na wengine wote ambao kwa namna moja au nyingine wameendelea kushirikiana na Serikali kuinua kiwango cha utoaji huduma za ustawi wa jamii nchini.


“Ninapenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Magufuli, ipo tayari kufanya kazi pamoja nanyi ili tuweze kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo 2030.”


Kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Uadilifu, Weledi na Uwajibikaji katika Utoaji wa Huduma za Ustawi wa Jamii Ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ni Nguzo katika kuelekea Uchumi wa Kati wa Viwanda.”


Waziri Mkuu amepongeza kwa kuanzisha utamaduni huo wa kukutana Watendaji wa Sekta ya Ustawi wa Jamii kwa kuwa hiko ni kiashiria kwamba kuna mabadiliko katika utendaji kwa kuzingatia kuwa mkutano huu haujawahi kufanyika toka mwaka 2006.


Mkutano huo wa siku tatu unajumuisha Maafisa Ustawi wa Jamii 164 kutoka mikoa yote Tanzania Bara, wadau wa maendeleo, wawakilishi wa wazee, watoto waishio katika mazingira hatarishi waliohitimu mafunzo ya VETA pamoja na watoto waliokuwa wakiishi mitaani ambao kwa sasa wameunda kikundi cha burudani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com