Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI UMMY MWALIMU ATAKA WAGANGA WAKUU HOSPITALI ZA SERIKALI KUWA WABUNIFU


Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewekeza kiasi cha Sh1.2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kitengo cha watoto katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Kujengwa kwa kitengo hicho kutaiwezesha JKCI kuwafanyia upasuaji wa kufungua vifua watoto 40 kwa mwezi kutoka 20 wa hapo awali pamoja na vyumba vinne vya madaktari wa kuona wagonjwa watoto wanaougua maradhi hayo kutoka kimoja cha awali.

Akizungumza baada ya ukaguzi wa kitengo hicho jana Jumapili Januari 20, 2019 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Rais Magufuli tayari ameidhinisha Sh500 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo ifikapo Januari 28, 2019.


Alisema kitengo hicho kinachotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu, kimegharimu Sh2 bilioni ambazo fedha nyingine Sh800 milioni zimetolewa na wafadhili Charity Baptism.

“Serikali awali iliweka Sh700 milioni na wiki hii mheshimiwa Rais ametoa Sh500 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi ili watoto wahamie katika jengo hili,” alisema Waziri Ummy.

Ummy alisema mwaka 2018 JKCI ilifanya operesheni nyingi zaidi kwa watoto hivyo anategemea mwaka huu zitaongezeka zaidi, “Hii itakuwa wodi ya kwanza kwa ajili ya watoto pekee kwa Afrika Mashariki walio wengi wanachanganya watoto na wakubwa.”

Katika hatua nyingine, Waziri Ummy amewaagiza waganga wakuu na wakurugenzi wote wa hospitali za Serikali nchini kuwa wabunifu katika kutatua changamoto katika maeneo yao ya kazi kama anavyofanya Mkurugenzi wa Taasisi ya Moya ya Jakaya Kikwete(JKCI),Profesa Mohamed Janabi.

Ummy Mwalimu alisema Profesa Janabi amekuwa akifanya kazi kubwa kutafuta wafadhili mbalimbali wa kuiwezesha taasisi hiyo, kupata miundombinu, Vifaa tiba pamoja na wataalam kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya kutoa huduma ya kitabibu na kutoa mafunzo pia kwa madaktari na wauguzi wa taasisi hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji JKCI, Profesa Mohamed Janabi aLIsema kitengo hicho kipya kilichoanzishwa pembeni mwa jengo hilo kitakuwa na vitanda 32 kutoka 11 vya awali.

“Watoto walikuwa na vitanda 11 pekee lakini kwa sasa tutakuwa navyo 32 na vitanda vya ICU vitakuwa 15,” alisema Profesa Janabi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com