Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

YANGA SC YAITOA BIASHARA UNITED KWA MATUTA, YATINGA 16 BORA ASFC


Yanga SC imefanikiwa kwenda hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya ushindi wa penalti 5-4 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.

Waliofunga penalti za Yanga SC ni Heritier Makambo, Paul Godfrey, Ibrahim Ajibu, Thabani Kamusoko na Matheo Anthony, za Biashara United zilifungwa na Lenny Kissu, George Makang’a, Derick Mussa, Kauswa Bernard, wakati Tariq Seif akapaisha ya nne.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Martin Saanya aliyesaidiwa na Abdallah Rashid na Rashid Zongo, Biashara United ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza 2-1.

Waziri Junior alianza kuifungia Biashara United kwa penalti dakika ya pili tu kufuatia beki Andrew Vincent ‘Dabte’ kumuangusha kwenye boksi George Makang’a.

Yanga SC wakasawazisha kwa penalti pia iliyopogwa na mshambuliaji wake Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe dakika ya saba kufuatia Frank Sekule wa Biashara United kumuangusha Nahodha, Ibrahim Ajibu.

Na Biashara United wakapata bao la pili dakika ya 41 kupitia kwa Innocent Edwin aliyemlamba chenga nzuri beki mkongwe Kelvin Yondan kabla ya kumchambua kwa shuti la kitaalamu kipa Ramadhani Kabwili.

Kipindi cha pili Yanga SC waliingia na mchezo wa kushambulia zaidi kusaka bao la kusawazisha na wakafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 73 kupitiakwa mshambuliaji wake Heritier Ebenezer Makambo aliyemalizia mpira ulipanguliwa na kipa Nourdine Balora baada ya krosi ya Mrisho Khalfan Ngassa.
 
Kocha Amri Said ‘Stam’ alichukizwa na kipa wake, Nourdine Balora baada ya bao hilo na akamtoa nafasi yake ikichukuliwa na Hassan Robert.

Kocha huyo alionekana akitoleana maneno makali na kipa huyo kabla ya kumsemea kwa refa Saanya aliyemuinua kwenye benchi na kumuamuru atoke kwenye eneo hilo. 

Yanga SC sasa itamenyana na Namungo FC ya Ruangwa mkoani Lindi ambayo iliitoa Mighty Elephant.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ramadhani Kabwili, Paulo Godfrey, Gardiel Michael, Kelvin Yondan, Andrew Vincent ‘Dante’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mrisho Ngassa, Pius Buswita/Thabani Kamusoko dk60, Heritier Makambo, Amiss Tambwe/Matheo Anthony dk76 na Ibrahim Ajibu. 

Biashara United; Nourdine Balora/Hassan Robert dk76, Taro Ronald/Kauswa Bernard dk67, George Makang’a, Waziri Junior/Tariq Seif dk63, Juma Mpakala, Frank Sekule, Innocent Edwin, Lenny Kissu, Wilfred Nkouzima, Derick Mussa na Abdulmajid Mangalo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com