AGPAHI YATOA MSAADA WA MAGARI YA MILIONI 186 KUSAIDIA UTOAJI WA HUDUMA ZA VVU NA UKIMWI MARA



Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa (kushoto) na Mkuu wa mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima, wakifungua moja ya magari yaliyotolewa na AGPAHI mkoani Mara kwa ajili ya kusaidia utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI katika halmashauri za wilaya za Bunda na Rorya, Februari 5,2019.


Mkuu wa mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima, akifungua moja ya magari hayo kwa ajili ya ukaguzi. Nyuma yake ni Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa.
Mkuu wa mkoa wa Mara, Mh. Adam Malima akifurahia wakati wa kufungua gari.
Mkuu wa mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima, akisaini ya kushuhudia mkataba wa makabidhiano ya magari hayo.
Mkuu wa mkoa wa Mara, Mh. Adam Malima, akisisitiza matumizi bora ya gari kwa uongozi wa halmashauri ya Bunda.
Mkuu wa mkoa wa Mara, Mh. Adam Malima, ndani ya moja ya magari yaliyotolewa na AGPAHI.
Mratibu wa AGPAHI mkoa wa Mara, Bi Alio Hussein, akisaini makubaliano ya makabidhiano ya magari hayo.
Picha ya pamoja baada ya magari kukabidhiwa kwa halmashauri za Bunda na Rorya
***
Asasi ya kitaifa inayolenga kutokomeza UKIMWI kwa watoto na familia, Ariel Glaser Pediatric AIDS Health Initiative (AGPAHI),leo imetoa msaada wa magari mawili yenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 186 kwa ajili ya kusaidia utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI katika halmashauri za wilaya za Bunda na Rorya, mkoani Mara.

Akikabidhi magari hayo aina ya Nissan Patrol kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, mjini Musoma, Februari 5,2019, Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk.Sekela Mwakyusa, amesema asasi hiyo imenunua magari hayo ili kukabiliana na changamoto ya usafiri hivyo kuboresha utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI katika halmashauri husika.

“Usafiri umekuwa ni changamoto kwa halmashauri nyingi. Kwa kutambua hilo, kwa awamu, tumekuwa tukizipatia halmashauri misaada ya vifaa vya usafiri kama vile magari, pikipipiki na baiskeli hivyo kwa awamu kwa kuzingatia upatikaji wa fedha na uhitaji wao. Mwaka jana pekee AGPAHI ilinunua vyombo vya usafiri vyenye jumla ya shilingi bilioni1.2,” anasema Dk. Mwakyusa.

Mkurugenzi Mtendaji amesema AGPAHI ambayo kwa sasa inahudumu katika mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu na Shinyanga n imuumini mzuri wa upatikanaji wa huduma bora za VVU na UKIMWI. 

Kwa mantiki hiyo kwa ufadhili wa watu wa Marekani kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) chini ya Vituo vya Kudhibiti Magonjwa na Kinga (CDC) ,AGPAHI imekuwa ikifanya mambo mbalimbali kuboresha utoaji wa huduma hizo.

“Ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na huduma bora za VVU na UKIMWI, tumefanyia ukarabati majengo 158 ya kutolea huduma ili kuwawezesha wengi kupata huduma hizo na katika mazingira mazuri, tumenunua vifaa tiba vyenye jumla ya thamani ipatayo sh. Bilioni 4 na kuviweka kwenye maeneo ya kutolea huduma katika mikoa tunayofanyia kazi,” amesema.

Aidha amesema kwa kutambua kuwa huduma hizo ni muhimu kutolewa na watu wenye utaalamu nazo, AGPAHI imesaidia watumishi 7,121 kupata mafunzo mbalimbali ya utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI. 

“Watumishi 457 waliwezeshwa kupata ajira hivyo kupunguza upungufu wa wafanyakazi wa kada ya afya nchini”.

Akizungumzia mafanikio yatokanayo na huduma za AGPAHI mkoani Mara, Dk. Sekela amesema kuwa asasi hiyo kwa kusaidiana na serikali imekuwa ikitoa huduma kwenye vituo 122 vya kutolea huduma na kupata mafanikio makubwa.

“Kuanzia Januari 2017 hadi Disemba mwaka 2018, tulifanikiwa kupima VVU watu 494,188 ambapo 15,748 walionekana kuwa na maambukizi. Watu14,804 ya watu hao walioonekana kuishi na VVU ambao ni sawa na 94% walianzishiwa dawa za kupunguza makali ya VVU,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI.

Kwa upande wa kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, Dk. Mwakyusa amesema AGPAHI iliendelea kusaidia utoaji huduma hizo mkoani hapa na katika kipindi hicho akina mama wajawazito108,696 walipimwa VVU ambapo 2,057 walionekana kuambukizwa. Wamama1,867 (asilimia 90.8) walianzishiwa dawa hivyo kufanikisha kuzaliwa kwa watoto 2,000 (asilimia 96.5) walizaliwa bila maambukizi.

Amesema katika kipindi hicho hicho cha Januari 2017 na Disemba 2018, watu 35,398 wanaotumia dawa za kupunguza makaliya VVU walipimwa kipimo cha wingi wa virusia mbapo 28,670 ambao ni sawa na 81% walionekana kuwa idadi ya virusi vilivyofubazwa.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Adam Malima, aliishukuru AGPAHI kwa msaada wake wa hali na mali katika kuboresha afya za watanzania, hususan za watu wanaoishi na VVU.

Mkuu huyo alisema kuwa AGPAHI imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia serikali kuboresha afya ya wananchi wake mkoani mwake.

“Ukienda sehemu nyingi za kutolea huduma hutaacha kuona kazi nzuri ya AGPAHI, kama siyo majengo waliyoyakarabati ili kuyawezesha kutoa huduma bora, basi utaona vifaa tiba, vitendea kazi mbalimbali na hata watumishi waliopata mafunzo au ajira kutokana na AGPAHI”,amesema Malima.

Akikabidhi magari hayo kwa halmashauri za Rorya na Bunda, Mkuu wa mkoa alizitaka halmashauri hizo kuhakikisha kuwa magari hayo yanatumiwa kwa shughuli iliyokusudiwa.

“Tunataka siku AGPAHI wakirudi kukagua kazi zao, basi waone kuwa magari haya yaliweza kutuongezea tija katika shughuli za VVU na UKIMWI", ameongeza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post