Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Zainab Telack ameipongeza Asasi ya kitaifa inayolenga kutokomeza UKIMWI kwa watoto na familia, Ariel Glaser Pediatric AIDS Health Initiative (AGPAHI) kwa jitihada inazozifanya katika kuboresha utoaji wa huduma za Virusi Vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI mkoani Shinyanga.
Mhe. Telack ametoa pongezi hizo leo Jumatano Februari 6,2019 wakati akipokea magari mawili aina ya Nissan Patrol yenye thamani ya shilingi milioni 186.5 yaliyotolewa na AGPAHI kwa ajili ya kusaidia utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI katika halmashauri za wilaya za Kahama Mji na Ushetu.
Alisema AGPAHI wamekuwa wadau bora katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI na kuwaomba kuendelea kushirikiana na serikali katika kuwahudumia wananchi.
Alisema kutokana na juhudi zinazofanywa na wadau wakiwemo AGPAHI kwa kushirikiana na serikali takwimu za maambukizi ya UKIMWI mkoani Shinyanga zimepungua kutoka asilimia 7.4 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 5.9 mwaka 2016/2017.
“Kazi mnayofanya ni ya kujenga familia za Watanzania,niwashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa mnaotupatia,naomba tuendelee kushirikiana”,alisema Mhe. Telack.
“Leo nimepokea magari haya mawili na sasa idadi ya magari yaliyotolewa na AGPAHI mkoani hapa tangu ilipoanza kazi zake,yanakuwa manne,naomba mtupatie pia magari kwa ajili ya Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga kwani napo bado wananchi wanahitaji elimu ya VVU na UKIMWI”,aliongeza Mkuu huyo wa mkoa.
Aidha aliahidi kuwa, magari hayo yatatumika kwa malengo yaliyokusudiwa huku akiwataka Wataalamu wa afya kutumia magari kuwafikia wananchi wengi zaidi yakiwemo maeneo ya wachimbaji madini na kuwaelimisha kuhusu masuala ya VVU na UKIMWI.
Akikabidhi magari kwa mkuu wa mkoa, Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa alisema magari hayo yatasaidia katika kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza tija katika kuboresha huduma za VVU na UKIMWI.
“Tunatambua kuwa wilaya ya Kahama ina kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU, ndiyo maana tumeona vyema tutoe magari Kahama Mji na Ushetu kwani uhitaji ni mkubwa ili kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI tukishirikiana na serikali”,alisema Dk. Sekela.
“Mbali na kutoa magari pia tulishatoa pikipiki na baiskeli. Aidha tumekarabati vituo vya kutolea huduma na tumewezesha ajira na mafunzo mbalimbali ya utoaji huduma za VVU na UKIMWI”,alisema.
Aidha alieleza kuwa, katika kipindi cha kuanzia Januari 2017 hadi Disemba 2018, AGPAHI imefanikiwa kupima VVU watu 905,724 mkoani Shinyanga ambapo watu 27,724 wanaoishi na VVU walianzishiwa dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs) katika vituo 107 vya kutolea huduma.
“Katika kipindi hicho pia akina mama wajawazito 140,173 walipimwa VVU ambapo 6,555 walionekana kuambukizwa.WAVIU wamama 6,481 (98.9%) walianzishiwa dawa na watoto 4,877 (96%) walizaliwa bila maambukizi”,alifafanua Dk. Sekela.
Magari hayo yamekabidhiwa na AGPAHI kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) chini ya Vituo vya Kudhibiti Magonjwa na Kinga (CDC).
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Zainab Telack akizungumza wakati Asasi ya AGPAHI ikikabidhi magari mawili yenye thamani ya shilingi milioni 186.5 kwa ajili ya kusaidia utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI katika halmashauri za wilaya za Kahama Mji na Ushetu. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa, kulia ni Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Muonekano wa magari yaliyo magari mawili yaliyotolewa na AGPAHI kusaidia utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI katika halmashauri za wilaya za Kahama Mji na Ushetu.
Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa akimweleza jambo Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack wakati akimkabidhi funguo za moja ya magari hayo ili akague.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Zainab Telack akijiandaa kuingia ndani ya gari wakati Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela akikagua gari. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Zainab Telack akiwasha gari ikiwa ni sehemu ya ukaguzi.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Zainab Telack akikabidhi ufunguo wa gari kwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Ushetu, Michael Augustino Matomora (wa kwanza kushoto mwenye suti nyeusi) na Mwenyekiti wa halmashauri ya Ushetu, Juma Kimisha (katikati).
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Zainab Telack akimkabidhi ufunguo wa gari Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Kahama Mji, Anderson Msumba (kushoto).
Kushoto ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Ushetu, Juma Kimisha akipokea kadi ya gari.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Zainab Telack na Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa wakibadilishana hati za makabidhiano ya magari.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Zainab Telack (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa wakisaini hati za makabidhiano ya magari mawili aina ya Nissan Patrol yenye thamani ya shilingi milioni 186.5.
Mratibu wa Mradi AGPAHI mkoa wa Shinyanga, Dk. Gastor Njau (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Ushetu, Michael Augustino Matomora nao wakisaini hati za makabidhiano ya magari.
Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa akimkabidhi Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack nakala ya Mpango Mkakati wa AGPAHI 2018-2022.
Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa (kulia) akieleza mafanikio ya AGPAHI hadi kufikia Septemba 2018 ambapo alisema watu 395,777 wanapatiwa huduma za VVU na UKIMWI katika vituo vya kutolea huduma katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara. Watu 248,000 wakiwemo watoto 13,600 wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dk. Rashid Mfaume akiishukuru AGPAHI kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika kutoa huduma za VVU na UKIMWI.
Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dk. Sekela Mwakyusa (kushoto) akiagana na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack baada ya kukabidhiana magari.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin