Mratibu wa Kudhibiti na Kupambana na Ukimwi mkoa wa Shinyanga, Dkt. Peter Mlacha.
Asasi ya kitaifa inayolenga kutokomeza UKIMWI kwa watoto na familia, Ariel Glaser Pediatric AIDS Health Initiative (AGPAHI) imeendesha warsha kwa Watoa Huduma za Virusi vya UKIMWI na UKIMWI mkoani Shinyanga ili kuwajengea uwezo kwa ajili ya kuboresha huduma katika vituo vya tiba na matunzo (CTC).
Mafunzo hayo ya siku tatu yamefunguliwa leo Februari 18,2019 na Mratibu wa Kudhibiti na Kupambana na Ukimwi mkoa wa Shinyanga, Dkt. Peter Mlacha na yameshirikisha washiriki 38 kutoka halmashauri za Kahama Mji,Ushetu,Kishapu, Msalala,Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga.
Watoa Huduma za Virusi vya UKIMWI na UKIMWI wanaoshiriki mafunzo hayo ni watu wanaoishi na maambukizi ya VVU (Waviu Washauri) waliojiweka wazi na huru kuwashauri watu wanaoishi na VVU katika masuala mbalimbali ikiwemo ufuasi mzuri wa dawa,kutoa ushauri nasaha,kujitolea kufuatilia na kufundisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha sambamba na kuhamasisha Waviu kujiunga katika vikundi ili kusaidiana na kupunguza unyanyapaa.
Akifungua Mafunzo, Dkt. Mlacha alisema miongoni mwa changamoto zilizopo mkoani humo ni wateja kupotea katika huduma hivyo kuwaomba watoa huduma hao kushirikiana na serikali kuwarudisha kwenye huduma ili waendelee kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU.
“Dhumuni la serikali yetu ni kutoa huduma bora kwenye vituo vya afya,na ili kufikia malengo haya ndiyo maana tumewaita ili tujengeane uwezo kwa ajili ya kuboresha huduma",alisema.
“AGPAHI ikishirikiana na serikali tutamfikia kila Mtanzania,lakini kwa kushirikiana nanyi ndiyo tutawafikia kwa urahisi zaidi,naomba tuendelee kushirikiana”,alieleza Dkt. Mlacha.
Kwa upande wao,Washiriki wa warsha hiyo walizitaja baadhi ya sababu zinazochangia wateja kupotea katika huduma kuwa ni kuhama hama kwa wafugaji,madereva wa magari,wafanyabiashara,wachimbaji madini,vituo vya afya kuwa mbali na wateja kutoa anuani ambazo siyo sahihi.
Aidha waliwataka baadhi ya viongozi wa dini kuacha kuwapotosha watu waliopata maambukizi ya VVU kwamba wakiombewa Virusi vinapotea mwilini na badala yake wawahamishe kutumia dawa za ARVs ili kunusuru maisha yao.
Mratibu wa Kudhibiti na Kupambana na Ukimwi mkoa wa Shinyanga, Dkt. Peter Mlacha akifungua warsha kwa Watoa Huduma za Virusi vya UKIMWI na UKIMWI mkoa wa Shinyanga ili kuwajengea uwezo kwa ajili ya kuboresha huduma katika vituo vya tiba na matunzo (CTC). Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mratibu wa Kudhibiti na Kupambana na Ukimwi mkoa wa Shinyanga, Dkt. Peter Mlacha akiwahamasisha washiriki wa warsha hiyo kuendelea kushirikiana na serikali kufuatilia wateja waliopotea katika huduma.
Washiriki wa warsha hiyo wakiwa kumbini.
Mratibu wa Huduma za VVU na UKIMWI katika jamii mkoa wa Shinyanga, Edwiga Zumba akitoa mada wakati wa warsha hiyo na kuwataka Waviu Washauri kutunza siri za wateja.
Mwezeshaji wa Huduma za VVU na UKIMWI katika jamii, Mwita Thomas akitoa mada ukumbini. Alisema Huduma za VVU na UKIMWI katika jamii ni huduma zinazojumuisha mkusanyiko wa huduma za zinazolenga uhamasishaji wa huduma za afya,uzuiaji wa maambukizo na muendelezo wa huduma ya tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU,Familia zao,jamii pamoja na watu walioko katika makundi maalumu.
Mwezeshaji wa Huduma za VVU na UKIMWI katika jamii, Mwita Thomas akielezea kuhusu huduma zinazojumuishwa kwenye huduma za VVU na UKIMWI katika jamii.
Daniel Richard kutoka kituo cha afya Chambo akichangia hoja wakati wa warsha hiyo.
Godfrey Mungo kutoka kituo cha afya Chamaguha akichangia hoja wakati wa warsha hiyo.
Consolatha Kapela kutoka kituo cha afya Samuye akizungumza wakati wa warsha hiyo.
Picha ya pamoja washiriki wa warsha Mwezeshaji wa Huduma za VVU na UKIMWI katika jamii, Mwita Thomas akitoa mada ukumbini.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin