Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATANGAZA NAFASI ZA AJIRA 4,549 ZA WALIMU

Serikali imetangaza nafasi za ajira 4,549 za walimu wa shule za msingi na sekondari katika mwaka wa fedha 2018/19 ili kupunguza uhaba wa walimu ulipo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo,amesema Serikali inajua kuwa kuna changamoto nyingi katika sekta ya elimu nchini hasa uhaba wa walimu hivyo itaajiri walimu ili kupunguza uhaba uliopo.

Hata hivyo Jafo amesema kuwa ajira hizo mpya kwa waombaji zinapaswa kuombwa kwa njia ya mtandao na mwisho wa kupokea maombi utakuwa Machi 15, mwaka huu.

”Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli inaendelea kuongeza idadi ya watumishi katika sekta ya umma kwa kutoa nafasi mbalimbali za ajira kwa vijana wa kitanzania katika sekta ya Elimu”amesema Jafo.

Waziri Jafo amesema kuwa Ofisi ya Rais Tamisemi inawatangazia walimu wenye sifa hizo kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao (Online Teacher Employment Application System-OTEAS).

Jafo amesema kuwa kwa walimu wa shule za msingi wanaotakiwa kutuma maombi ni wenye sifa za kitaaluma Daraja la IIIA wenye Astashahada ya ualimu, na wenye daraja la IIIB wenye Stashada (Diploma ya ualimu katika masomo ya Kingereza, Uraia, Historia, Jiografia na kiswahili.

Aliongeza kuwa walimu wenye sifa ya Daraja la IIIC wenye shahada ya ualimu kwa masomo ya Kingereza,Uraia,somo la ziada,Historia,Geographia na Kiswahili.

Jafo ametangaza kundi jingine lenye sifa ni Mwalimu mwenye Daraja la IIIC na mwenye mahitaji maalum aliyehitimu Shahada kwa masomo ya English,Uraia,somo la ziada,Historia,Geographia na kiswahili.

Kwa walimu wa sekondari Waziri Jafo amesema kuwa wao wanaotakiwa kufanya maombi ni Mwalimu wenye Daraja la IIIC mwenye Shahada ya ualimu aliyesomea Elimu maalum.

Jafo amesema wengine ni wenye Daraja la IIIB wenye Stashahada (Diploma) ya ualimu waliosomea Elimu maalum na mwalimu Daraja la IIIB mwenye Stashahada ya ualimu somo la Mathematics, Biology, Physics,na Chemistry.

Amesema wengine wenye sifa za kuomba ni mwalimu daraja la IIIC mwenye shahada ya ualimu somo la Agriculture Science, na mwalimu wa Daraja la IIIC mwenye Shahada ya ualimu somo la Home Economics na mwalimu Daraja IIIC mwenye Shahada ya ualimu somo la Physics, Mathematics, Chemistry na Biology.

Aidha Jafo ameongeza kuwa walimu wengine ni wa Daraja IIIC wenye shahada ya ualimu somo la Book keeping, Commerce, Accounts na Economics na mwalimu daraja la IIIC mwenye Shahada ya ualimu somo la English, Civics na General Studies.

Hata hivyo Jafo amesisitiza kuwa waombaji wenye sifa zote hizo wanatakiwa kuwa watanzania, wawe wamehitimu kati ya mwaka 2014 hadi 2017 isipokuwa kwa kundi maalum la wahitimu wa elimu ya ualaimu wa masomo ya Fizikia na Hisabati.

Jafo amesema kuwa sifa nyingine ya jumla kwa muombaji asiwe na umri zaidi ya miaka 45, na wakati wa kutuma maombi walimu ambao waliwahi kutuma na hawajaajiriwa wanapaswa kutuma upya.
Na.Alex Sonna/Fullshangwe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com