Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BENKI KUU YAZINDUA MFUMO WA MALIPO YA PAPO KWA PAPO

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua mfumo mpya wa malipo ya fedha kwa njia ya kielektroniki utakaowezesha utumaji wa huduma za kifedha kutoka katika taasisi moja kwenda nyingine.


Pamoja na kurahisisha utumaji wa fedha, pia utaondoa urasimu na udanganyifu kwa taasisi za fedha.


Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuzindua mfumo huo, Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa wa BoT, Benard Dadi, alisema mfumo huo pamoja na kurahisisha utumaji wa fedha, pia utasaidia benki hiyo kupata taarifa za kifedha katika kila benki badala ya kusubiri kupelekewa taarifa hizo na taasisi za benki.


Kwa mujibu wa Dadi, pia utasaidia kuonyesha kiwango cha mapato ambacho serikali inapaswa kupata kupitia taasisi za fedha.


Kadhalika, alisema pia utapunguza matumizi ya fedha taslimu na kuondoa usumbufu ambao umekuwa ukitokea wa kukosea taarifa za kifedha ikiwamo majina na taarifa nyingine muhimu.


“Mfumo huo utasaidia kuonyesha kila muamala unaofanyika katika kila kampuni nyingine, kwa hiyo kutusaidia kujua miamala ni mingapi kwa siku, kwa mwezi, kwa mwaka, kuleta udhibiti ndani ya BoT, badala ya kwenda kwenye kampuni kwenda kuomba taarifa, hizo taarifa tutakuwa nazo, tutajua serikali inapata ushuru kwa kiasi gani kwa usahihi zaidi bila kutegemea mpaka ifike mwisho wa mwezi ndio tupewe taarifa kujua serikali imepata ushuru kiasi gani,” alisema Dadi na kuongeza:


“Vyote hivyo vitarahisishwa sana kupitia mfumo huu na kufanyika miamala utakuwa unachukua muda mfupi ndani ya sekunde mbili au tatu kumfikia mteja na pia itasaidia kupunguza gharama. Mfumo huu unajengwa ndani ya miezi 18 na utatumia wataalamu kutoka BoT,” alisema Dadi.


Sosteness Kewe, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), alisema mfumo huo mpya utakuwa na manufaa makubwa kwenye uchumi wa nchi, wananchi wa kawaida, wafanyabiashara na wakulima kwa sababu utakapoanza kufanya kazi utasaidia kupunguza gharama za utumaji wa fedha pamoja na kutoa taarifa za watu wote wanaotumia huduma za kifedha.


Alisema taarifa hizo pia zitasaidia taasisi za fedha kuongeza ufanisi namna ya kuboresha huduma kwa wateja.


“Tunajua wengi tunatumia mfumo wa fedha taslimu ambao ni gharama kubwa, lakini mfumo huu wa kutuma pesa kwa haraka utaepusha mengi, kwa mfumo wa sasa unatakiwa uende benki ukachukue pesa au umtume mtu au umtume boda boda, lakini kwa mfumo huu ambao BoT umezindua utarahisisha miamala mbalimbali kulipa au kupokea pesa kiurahisi hasa wafanyabiashara, wakulima kufanya miamala kwa urahisi zaidi, hawatakuwa na haja ya kulipa fedha taslimu,”alisema Kewe.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com