Jamaa mmoja aliyeingia kwenye nyumba iliyotelekezwa nchini Marekani ili avaute bangi amepatwa na mshtuko asioutarajia baada ya kukutana na Chui mkubwa aina ya Tiger ambaye alikuwa ametelekezwa.
Polisi jijini Houston, Texas wamesema awali bwana huyo alipowapigia simu walidhani kuwa yupo kwenye njozi (baada ya kuvuta bangi).
Lakini walipofika walimkuta Tiger mkubwa amefungiwa ndani ya kizimba.
Hakukuwa na alama yeyote iliyoonesha kuwa kuna watu waliokuwa wkiishi kwenye jengo hilo, japo kulikuwa na nyama mbichi karibu na kizimba hicho.
Polisi sasa wanasema watafanya uchunguzi ili kubaini namna gani mnyama huyo alifika hapo.
Wameeleza kuwa "raia mwema" ambaye aligundua uwepo wa tiger huyo hakuwa akiishi kwenye nyumba hiyo, na aliingia tu ili "avute bangi".
"Tuliwauliza iwapo kama wamelewa dawa za kulevya (bangi) ama kweli wamemuona tiger," msemaji wa polisi amewaambia wanahabari.
Polisi pia wameeleza kuwa kizimba hicho hakikuwa madhubuti, na kilikuwa kimefungwa na bisbisi na kamba ya plastiki.
Japo mnyama huyo hakuwa mwenye hasira, ilibidi kwanza apigwe dawa ya usingizi kabla ya kumtoa kwenye nyumba hiyo na kupelekwa kwenye maskani ya wanyama.
Tigers ni aina ya Chui wanaopatikana Kusini na Kusini Mashariki mwa Asia na mashariki ya mbali ya Urusi. Ni wanyama ambao wapo katika hatari ya kupotea. Inakadiriwa kuwa wamebaki 4,000 tu mwituni.
Chanzo - BBC