Wakazi wa kijiji cha Leleshwa kaunti ya Laikipia nchini Kenya wameachwa vinywa wazi huku wakitizama fisi akimshambulia na kumuua mvulana mwenye umri wa miaka 17 nyumbani kwao.
Mvulana huyo aliripotiwa kushambuliwa nyumbani kwao na mnyama huyo majira ya saa kumi na moja alfajiri alipokuwa akijiandaa kwenda shuleni.
Babake mwathiriwa alikuwa chumbani mwake akiwa amelala huku mamake akiwa jikoni akiandaa kifungua kinywa ambaye pia alivamiwa na fisi huyo na kuachwa na majeraha mabaya sana.
Wazazi wake walijaribu kumuokoa mtoto wao lakini pia wao walishambuliwa na kuachwa na majeraha mabaya.
Majirani walifika nyumbani kwa mwathiriwa ila hawakuweza kumuokoa mvulana huyo wao pia walifukuzwa na fisi huyo kila walipojaribu kumnusuru mvulana huyo.
Maafisa wa shirika la huduma kwa wanyama pori KWS waliofika nyumbani kwa waathiriwa walisema fisi huyo ni mmoja wa wanyama pori waliotoroka msituni kufuatia moto uliozuka.
Afisa anayesimamia mbuga ya wanyama ya Laikipia West Mohammed Madela alisema, wanyamapori kadhaa wameripotiwa kuvamia makazi ya binadamu na wanashughulikia suala hilo.
Wazazi wa mvulana huyo walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Nyahururu ambapo wanaendelea kupokea matibabu.
Chanzo - Tuko blog