Hatimaye mwili wa Frank Kapange (22) leo Jumanne Februari 26,2019 umechukuliwa na familia yake katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya baada ya kukaa mochwari miezi nane na siku 22.
Mwananchi lililokuwapo hospitalini limeshuhudia baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu walifika saa 3:30 asubuhi ambapo walichangishana fedha kwa ajili ya kusaidia shughuli za msiba.
Akizungumza hospitalini hapo, msemaji wa familia, Julius Kapange amesema wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuamuliwa na Mahakama kuwa wazike ndani ya wiki moja la sivyo jiji lingezika.
“Leo tumefanikiwa kuchukua mwili wa kijana wetu, tunaenda kuzika kijijini kwetu Syukula Rungwe sababu ya kufanya hivyo ni kwamba Mahakama ilitutaka tuzike kabla ya wiki moja.”
“Hivyo tukaona ni vyema tufanye hivyo kuliko kuendelea kumtesa mwanetu lakini mpaka tumefika hatua hii Mahakama haijatutendea haki katika kuamua kesi yetu,” amesema Kapange.
Kapange amesema siku ya Jumapili ya Februari 24,2019 waliitwa na mkurugenzi wa hospitali ya Rufaa ambapo waliambiwa wachukue mwili wa kijana wao na gharama za kuhifadhia maiti hiyo kwa muda wote wamesamehewa.
“Sisi tulienda mahakamani kuomba mwili wa mtoto wetu uchunguzwe kwani kifo chake kilikuwa ni cha utata na siyo kususia kama wengine wanavyosema na baada ya mazishi tutaendelea kufanya shughuli zingine za kimaendeleo,” amesema Kapange.
Akizungumza kwa njia simu mkurugenzi wa hospitali hiyo, Godlove Mbwanji amesema wameamua kusamehe gharama za kutunzia maiti hiyo kwa muda wote ili fedha ambazo waliziandaa zikatumike kwenye msiba.
Frank alifariki Juni 4, 2018 huku kifo chake kikigubikwa na utata kutokana na mazingira yake baada ya ndugu kudai kijana wao ambaye alikuwa ni mfanyabiashara wa nguo za mitumba soko la Sido jijini Mbeya kufariki kwa kipigo akiwa mikononi mwa polisi hivyo ndugu waligoma kumchukua na kwenda kumzika.
Kutokana na ndugu hao kuona ukakasi wa kifo cha kijana wao walitaka kujiridhisha pasipo shaka juu ya kilichosababisha hivyo wakafungua shauri Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya itoe amri ya kufanyika kwa uchunguzi rasmi wa kisheria wa kifo cha kijana wao lakini mahakama hiyo Agosti mwaka jana ilitupilia mbali shauri hilo baada ya kuona kukosa mashiko na kuamuru mwili huo kuzikwa na ndugu wanahitajika kubeba gharama zote za mazishi.
Ndugu walidai kutoridhika na uamuzi huo, wakaamua kukataa rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambayo nayo Novemba 2018 ilitoa uamuzi wa kuifuta kesi hiyo baada ya kujiridhisha kwamba mlalamikaji hakufuata taratibu zilizopaswa wakati wa kufungua kesi hiyo.
Na Ipyana Samson, Mwananchi
Social Plugin