Waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Ndani alipata ajali katika eneo la Migori wilayani Iringa katika Barabara ya Dodoma–Iringa ambako alikuwa safarini kutoka Iringa kwenda mkoani Singida jana asubuhi.
Akizungumza kwa taabu akiwa amelazwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini hapa, Mwigulu alimshukuru Mungu kwa kutoka mzima kwani dereva wake aligonga punda waliokuwa wakivuka barabara katika eneo hilo.
Akizungumzia mkasa huo, Mwigulu alisema: “Nilikuwa natoka Iringa nakwenda Singida, nilikuwa naenda kwenye kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa, sikuwa naangalia mbele nadhani nilikuwa nazungumza na simu kama sikosei… ghafla wakakatiza punda kama sikosei walikuwa watatu.”
Aliongeza: “Nilishtuka tu dereva alivyotoa ishara kwamba kuna kitu cha hatari kwa hiyo ilikuwa ni kitendo cha kufumbua macho hapo hapo na gari ikawa imepinduka.
“Waligongwa wale punda watatu, mmoja alikuwa anamalizia barabara na mwingine alikuwa anaanza kuvuka barabara na mwingine alikuwa katikati, kwa hiyo hakukuwa na uwezekano wa kukwepa.
“Nilivyoona hivyo nilisikia kelele moja kubwa ya kugonga na baada ya hapo, sikuona tena mbele kwa sababu ghafla niliona mbele yangu pamekuwa padogo na kulikuwa na moshi unafuka.
“Mwanzo sikuona kama nimeumia nikamuuliza mwenzangu unaendeleaje? Nikamwambia tunaweza kutoka akaniambia ngoja kwanza kwani moshi mkubwa ulikuwa unafuka nikawa naona kama vile kuna hitilafu kubwa ya moto kwani kulikuwa na moshi na nilikuwa nimebananishwa,” alisema.
Alisema alipotoka ndani ya gari aliona kifua kinambana huku akisikia maumivu makali katika mguu wa kulia.
“Na nilipotoka kifua kilikuwa kinauma, kiuno na mguu, nashukuru nimepokewa hapa na nimepewa huduma haya maumivu ya kubana yaliyokuwa yakinisumbua naona sio sana yamebaki maumivu ya mwili tu,” alisema.
Alimshukuru Mungu kwa kutoka salama kwani alikuwa akiona kifo kipo mbele yake. “Mungu ni mwema, Mungu ni mwema,” alisema mwanasiasa huyo kijana.
Akizungumzia dereva wake, alisema hali yake ni nzuri na aliwaagiza wasaidizi wake wampigie kujua hali yake. Mwigulu aliwataka Watanzania kuendelea kumuombea ili apone. “Naomba waniombee Mungu ni mwema ametunusuru, Mungu ni mwema ametunusuru,” alisema Mwigulu.
Kwa upande wake, dereva wa gari hiyo, Johnson Malesi akizungumza kwa njia ya simu na gazeti la Habarileo, alisema ajali hiyo ni kama ya maajabu kwani imetokea katika eneo la wazi.
Alisema ilitokea saa 2.45 asubuhi katika eneo la Migori mkoani Iringa ambako alikuwa akikwepa punda waliotokea ghafla barabarani.
“Ilikuwa saa 2.45 asubuhi tulikuwa tunatoka Iringa kupitia barabara ya Mtera na tulikuwa tumefika Migori na tulikuwa tumeachana na kijiji na kulikuwa hakuna makazi ya watu.