Mahakama Kuu imeahirisha kesi ya kikatiba kuhusu kinga ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na mamlaka ya Bunge kuwahoji watu wanaotuhumiwa kulidhalilisha Bunge.
Kesi hiyo ya kikatiba namba 1/2019, imefunguliwa mahakamani hapo masjala kuu na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Jaji Firmin Matogolo, Jaji Benhajj Masoud na Jaji Elinaza Luvanda na kuahirishwa hadi Machi 26, mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.
Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa ACT Wazalendo, anawakilishwa na Wakili Fatma Karume, waliiomba mahakama hiyo itoe tafsiri ya kinga ya CAG iliyopo kikatiba na pia kutoa tafsiri ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge katika kushtaki watu wanaosemekana kudharau Bunge.
Katika kesi hiyo, wanaiomba mahakama itamke na kuamuru kwamba amri ya Ndugai kwa CAG ni kinyume cha Katiba kwa kukinzana na masharti ya Ibara za 26 (1), 18(a) (b) na (d) za Katiba ya Tanzania na kwamba wito huo ni batili.
Waleta maombi hao pia wanaiomba mahakama hiyo zuio la kudumu kumzuia Ndugai, watumishi wake au wakala wake kutokuchukua hatua yoyote ikiwamo kuamuru au kuelekeza mtu yeyote kumkamata au kumchukua CAG kwenda Dodoma kuhojiwa na Kamati ya Bunge kuhusu kauli yake hiyo.
Hata hivyo, CAG alihojiwa kuhusiana na kauli yake aliyoitoa akiwa nchini Marekani ya kudai kuwa Bunge la Tanzania ni dhaifu kulingana namna ambayo taarifa zake za ukaguzi zinavyofanyiwa kazi.
Social Plugin