Mtaalamu wa uchunguzi akiwa kwenye nyumba ambayo mwili wa mwanamke aliyetoweka miaka 20 iliyopita, ulikutwa ukiwa ndani ya friji. AFP
Taharuki imetanda katika kijiji kidogo nchini Croatia ambako mwili wa mwanamke aliyekuwa ametoweka umepatikana kwenye friji ya dada yake mwishoni mwa wiki, jambo la kutisha ambalo limezingira kesi hiyo iliyodumu kwa miaka 20.
Jasmina Dominic alitoweka mwaka 2000 wakati akiwa mwanafunzi mwenye umri wa miaka 23.
Jumamosi mwili wake ulipatikana ukiwa umeganda ndani ya friji iliyokuwa ghorofa ya kwanza ya nyumba ya dada yake anayeitwa Smiljana Srnec katika kijiji cha Palovec, ambacho ni kidogo lakini kilicho na uchumi mzuri na nyumba za ghjorofa mbili.
Kujulikana kwa suala hilo kumetisha jamii, huku waendesha mashtaka wakimnyooshea kidole dada huyo ambaye amekuwa akiishi na mwili huo kwenye friji kwa miaka hiyo yote.
"Smiljana Srnec ni nani?", moja ya magazeti makubwa nchini Croatia la Vecernji List liliuliza katika kichwa cha habari leo, likichapisha picha ya mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 45 akiwa na nywele fupi, miwani huku akitabasamu.
hali ya wasiwasi imetanda kijiji cha Palovec, ambacho kina watu wapatao 900, wengi wao wakiwa na mashamba na wengine wanafanya kazi katika kiwanda cha viatu kilicho karibu na kijiji.
Mapazia yamefungwa katika nyumba hiyo nyeupe ya Srnec wakati gari limeendelea kuwa katika maegesho.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, aliyeuona mwili huo kwenye friji ni mkwe wa Srnec ambaye baadaye Jumamosi aliitaarifu polisi.
"Hakuna mtu kijijini anayeweza kulala. Wote tumepata na mshtuko," alisema mwanaume mwenye umri wa miaka 62 ambaye ni jirani wa Srnec aliyekataa jina lake kutajwa.
Mtu huyo alisema ameombwa na polisi awe shahidi.
"Kwa sekunde mbili niliuona mwili ukiwa umejikunja ndani ya friji na mikono yake imekumbatia mwili," alisema kabla ya kurejesha kumbukumbu ya madada hao wawili.
"Walikuwa wanatofautiana. Jasmina alikuwa mtu mzuri, asiyependa makuu na alisoma Zagreb, alikuwa mchapakazi, wakati Smiljana hakuwa wa namna hiyo, hakuwa anafanya vizuri shuleni," alisema.
Ni jambo la kutatanisha," alisema jirani mwingine, akitingisha kichwa kuonyesha kutoamini kilichotokea.
Tovuti inayoweka rekodi za watu wanaotoweka inaonyesha picha ya Dominic akiwa na nywele fupi. Tovuti hiyo inasema alipotea Agosti 2000, mwaka ambao aligundulika kuwa haonekani Chuo Kikuu cha Zagreb wala kwenye kazi za wanafunzi.
Kwa mujibu wa habari ziloizopatikana kijijini hapo, ndugu hao wawili walikuwa wakitumia nyumba moja wakati wazazi wao wanafanya kazi nje.
Familia ya Dominic haikutangaza kutoweka kwake hadi mwaka 2005, wakati ilipoiambia polisi kuwa aliwaaga kuwa alikuwa anakwenda kufanya kazi kwenye meli.
Polisi walisema walifanya msako kwenye nyumba hiyo bila ya mafanikio na kuamua kutumia mfumo wa kubaini uongo.
Tangu wakati huo baba yao alifariki, wakati mama yao anafanya kazi nchini Ujerumani, kwa mujibu wa majirani.
"Ni kama muda umesimama," alisema meya wa manispaa hiyo, Valentino Skvorc alipoongea na AFP kuzungumzia tukio lililotokea katika kijiji hicho ambako wakazi hupenda kujifungia majumbani na hawako tayari kuzungumza.
"Mambo kama haya mara nyingi hutokea katika vipindi vya televisheni, lakini sasa uhalifu umefanywa na jirani... watu wameshtushwa," aliongeza Skvorc.
Katika baa moja ya kijijini hapo, Stjepan, fundi mstaafu, alitoa maelezo yanayoweza kuwa ya kweli.
"Labda kilikuwa kifo cha bahati mbaya, inawezekana wazazi walijua," alisema Stjepan mwenye umri wa miaka 60 huku akinywa bia.
"Kama Smiljana alijua kuhusu huo mwili wakati wote huo, labda ni ugonjwa. Alikuwa akiupita (kwenye friji) kila siku," alisema.
Chanzo - Mwananchi
Social Plugin