Mwanamke aliyehusika kumfanyia ukatili mtoto wa miaka minane kwa kumchoma na kisu chenye moto mkali sehemu za mapaja anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kwa mahojiano.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Hamis Issah amesema mwanamke huyo mkazi wa kijiji cha Mbomai chini, tarafa ya Tarakea wilayani Rombo alifanya tukio hilo Februari 2, 2019
"Tukio hili lilitokea Februari 2, 2019 kata ya Mbomai chini, majira ya saa 3 usiku na aliyefanyiwa kitendo hicho cha kikatili ni mwanafunzi wa darasa la pili Shule ya Msingi Tarakea, mtuhumiwa alichukua kisu cha moto na kumchoma mtoto huyo sehemu za mapaja kwa madai ya kwenda kucheza na watoto wenzake," amesema Issah.
Ameongeza: "Siku chache baada ya kufanyiwa tukio hilo mwendo wa mtoto huyo ulibadilika baada ya walimu kubaini kuwa mtoto huyo anashida na alipoulizwa kwa nini anatembea kwa shida alipandisha suruali aliyokua amevaa na kuonyesha sehemu alizochomwa na moto, ndipo walimu walipomchukua na kumpeleka kituo chetu cha polisi, mhusika tumeshamkamata na atapandishwa mahakamani," amesema Issah.
Mwanafunzi huyo anapata matibabu katika kituo cha afya cha Tarakea wilayani humo.
Na Janeth Joseph,Mwananchi
Social Plugin