Jeshi la Polisi mkoani Rukwa limethibitisha uwepo wa tukio la uwepo wa kiumbe cha ajabu katika maeneo ya shule ya Msingi Kalalasi iliyopo Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa, hali iliyozua taharuki kwa wanafunzi na walimu.
Kimwonekano, kiumbe hicho kinafananishwa na binadamu ila tu tofauti ni kuwa ni kidogo na kina urefu kati ya sentimita 12-15 tu.
Akizungumza na Daily News Digital leo asubuhi, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Rukwa, George Kyando amekiri kutokea kwa tukio hilo Jumanne wiki hii (Februari 5, 2019).
Kamanda ameeleza kuwa hadi sasa haijajulikana asili ya kiumbe hicho japo wakazi wa maeneo ya jirani na shule hiyo wameanza kulihusisha tukio hilo na ushirikina.
“Wengi wanahusisha na imani za kishirikina lakini sisi kama Jeshi la Polisi bado tunachunguza tujue kama ni binadamu au ni kitu gani maana kimofolojia ni kama mtu kina umbo la binadamu lakini sio binadamu wa kawaida.
“Kwa hiyo tumekikabidhi kwa wataalamu wa afya ili waweze kukifanyia kiumbe hiki utafiti kama huyu ni binadamu au ni kitu gani,” amesema Kamanda Kyando.
Kwa Upande wake shuhuda wa tukio hilo aliyefahamika kwa jina la Nicodemus Kapele amesema kuwa kiumbe huyo alionekana maeneo ya shule hiyo nyakati za asubuhi na kuzua taharuki miongoni mwa wanafunzi na walimu shuleni hapo hali iliyopelekea wanafunzi kuanza kukishambulia kiumbe hicho kwa mawe na kufanikiwa kukiua.
Mwalimu aliyekuwa zamu siku hiyo, Thomas Stephano ambaye alikuwa zamu siku hiyo alieleza kuwa siku ya tukio (Jumanne) alishangaa kuona kuwa muda wa mapumziko umekiwisha (saa 4:30 asubuhi) ila cha kushangaza wanafunzi bado walikuwa nje kwenye kikundi.
“Ilibidi niwafuate kuona nini kilikuwa kinafanyika kufika tu nikakuta wakikiua kiumbe hicho. Tulikimwagia maji tukione vizuri maana niliwaambia usikute ni chura…wao wakasema ni binadamu. Kweli, baada ya kumwagiwa maji, kiumbe huyo ana umbile la binadamu,” ameeleza mwalimu huyo ambaye amefundisha shule ya Msingi Kalabasi kwa miaka minne sasa.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Billy Philipo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ila hakuwa tayari kutoa maelezo zaidi kwa kile alichodai kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kina kwa kuwa uchunguzi unaendelea.
Na Ombeni Utembele - Habarileo