Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFULI : SIJAINGILIA MUHIMILI WA MAHAKAMA WALA BUNGE


Rais John Magufuli ameueleza umma kwamba, katika uongozi wake hajawahi kuingilia kazi za muhimili wowote. 

Akizungumza leo tarehe 6 Februari 2018 kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam amesema, hajaingilia muhimili wa Mahakama wala Bunge.

“Katika uongozi wangu, mimi nimejitahidi sana kutoingilia muhimili wowote, sijaingilia muhimili wa Bunge. Hata mtu akikutukana unazima Tv (televisheni),” amesema Rais Magufuli na kuongeza; “sijaingilia muhimili wa mahakama.”

Ameitaka mahakama pia kutokubali kuingiliwa na mammlaka yoyote.

“Najua nina fahamu kuwa wapo wanaoingilia kwa hasira tu lakini nyie musiruhusu kuingiliwa,” amesema na kuongeza; Kila muhimili ujisimamie wenyewe kwa mujibu kwa Katiba ya Nchi.

Kwenye maadhimisho hayo Rais Magufuli amesema, serikali itaendelea kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na mhakama na kwa sasa inaendelea kushughulikia changamoto hizo.

“Changamoto zinazowakabili zisiwakatishe tamaa, hakuna kazi isiyo na changamoto. Hata tukimaliza za sasa zitajitokeza zingine,” amesema.

Rais Magufuli ameshauri wananchi wasome sheria ili kuweza kuzijua na kuwa, idara za mahakama na wadau wasaidie wananchi kutafsiri sheria.

“Nawasihi wananchi wasome sheria walau kwa uchache, idara ziwasaidie wananchi kutafsiri kwa lugha ya Kiswahili,” amesema na kuwaomba wananchi kutojichukulia sheria mkononi.

Rais Magufuli ameonesha kukerwa na tabia ya baadhi ya wapelelezi wanaopeleleza kesi zilizo na vidhibiti vilivyo wazi.

“Mtu unakuta ameshikwa na meno ya tembo, dawa za kulevya halafu eti upelelezi unaendelea. “Eti lazima tupeleke kwa Mkemia Mkuu na yanapoendelea kukaa huko wanasema ni majivu.”

Kiongozi huyo wa nchi amewataka majaji, mawakili kutenda haki kwa kuwa, wanaposimamia haki kazi yao inapata Baraka kutoka kwa Mungu.

“Wapelelezi kapelelezeni haraka, unapokiona kitu kipo unakwenda kupeleleza nini? Mtu ameiba na kitu anacho bado unakwenda kupeleleza.

“Unakwenda kupeleleza ili kujua wakati anaiba alikuwa ameinama ama amelala?” amehoji Rais Magufuli.

Amesema, wanasheria wana pande mbili, upande wa mshitaki na mshitakiwa na kwamba, wakati mwingine wanasheria huzungumza namna ya kuruka vipengele ili mshtakiwa aachwe huru.

“Mjue kuwa hamzikosei roho zenu tu bali mnamkosea Mungu. Kesi zingine zina ushahidi wa kutosha lakini zinafutwa,” amesema Rais Magufuli.

Amemsifu Prof. Ibrahim Juma, Jaji Mkuu kwa kueleza ukweli kuhusu changamoto za mahakama ambapo ameahidi kuzifanyia kazi kadri atavyoweza kupata wasaa.

“Ndio maana nikakwambia baada ya kumaliza hotuba yako, unikabidhi ili niendelee kupitia na nitayoweza kutatua haraka nitatue na mingine yanaweza kusubiri mpaka pale hali itakaporuhusu,” amesema.

Rais Magufuli amesema, ni muhimu kujenga jamii yanye kuheshimu haki, kudumisha amani na kuondoa migogoro kwenye jamii.

“Tupo hapa leo na tumekaa kwa amani kwa kuwa, zipo sheria zinatulinda, zisingekuwepo pengine tusingekuwa hivi leo,” amesema.
Chanzo - Mwanahalisi Online

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com