Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group Joseph Kusaga amesema kwamba msiba wa Ruge hautakuwa wa majonzi kama ilivyozoeleka, bali itakuwa ni kusherehekea maisha yake kama ambavyo mwenyewe alitaka iwe.
Kusaga amezungumza hayo akisema kwamba kabla Ruge hajafariki, aliwahi kusema kuwa ikitokea siku amekufa, basi watu wasihuzunike sana, bali washerehekee maisha yake na vile alivyo vifanya wakati yupo hai.
“Kuna kitu alikuwa akisisitiza, kwamba ikitokea bahati mbaya Mwenyezi Mungu amemchukua, tu-'celebrate' maisha yake, tu-'celebrate' alivyovifanya, kwa hiyo tutaanza maombolezo lakini yatakuwa ku-'celebrate' mazuri aliyoyafanya, hii alisisitiza wazi kabisa, na mimi kumpa heshima hiyo ni lazima tu-'celebrate' mengi mazuri aliyoyafanya”, amesema Kusaga.
Akiendelea kuzungumzia hilo Joseph Kusaga amesema kwamba Ruge amefanya mengi mazuri ambayo yalifaa kutunukiwa, huku akitoa shukrani kwa serikali kwa kuwa nao bega kwa bega, kwenye kipindi hiki kigumu kwao.
“Inaweza ikawa sio wakati mzuri wa kusema mengi, lakini Watanzania inabidi tujifunze kutoa tuzo au kitu chochote kizuri kwa mtu aliyefanya mambo mazuri, amefanya mengi mazuri kwenye tasnia hii na burudani, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa serikali na viongozi wote ambao wamekuwa kwa kiasi kikubwa wamekuwa wako karibu sana kutu suport, ili kuhakikisha tunamponya na maisha yake yanaendelea”, amesema Kusaga.
Ruge Mutahaba amefariki jioni ya Februari 26 huko Afrika Kusini, akipatiwa matibabu ya figo aliyokuwa akisumbuliwa nayo.
Social Plugin