Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUNDU LISSU AMJIBU BALOZI WA TANZANIA UJERUMANI

Siku chache baada ya Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk Abdallah Possi kutoa taarifa ya kumjibu Tundu Lissu kutokana na madai aliyoyatoa alipohojiwa na kituo cha televisheni cha Deutsche Welle nchini humo, mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema) ameibuka na kumkosoa balozi huyo.

Katika maelezo yake, Dk Possi alimtaka Lissu kurudi Tanzania ili kutoa ushirikiano wa uchunguzi unaofanywa na Polisi.

Hata hivyo, Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 mchana wa Septemba 7, 2017 jijini Dodoma amesema uchunguzi huo hauhitaji yeye wala dereva wake kuwapo.

“Sheria ya kusaidiana katika masuala ya jinai iliyotungwa na Bunge la Tanzania, imeweka utaratibu wa namna ya kupata ushahidi au mtuhumiwa aliyeko nje ya Tanzania,” amesema Lissu kupitia ujumbe aliotutuma Mwananchi.

“Kwa mujibu wa sheria hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Tanzania anatakiwa kuomba msaada wa nchi aliko shahidi au mtuhumiwa huyo ili kupatikana ushahidi au mtuhumiwa anayehitajika kwa uchunguzi wa kijinai,” ameongeza. 

Lissu amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania hajawahi kuomba msaada wa Serikali ya Kenya, kwa kipindi chote cha miezi minne alichokuwa Hospitali ya Nairobi wala kwa Serikali ya Ubelgiji tangu alipokwenda Januari 6, 2018 kwa matibabu zaidi.

“Kauli hii, ambayo imerudiwa rudiwa sana na Serikali, ina maana kwamba kama mimi na dereva wangu tungeuawa siku ya shambulio hilo, basi kusingekuwa na uchunguzi wowote?” alihoji.

Amesema yeye na dereva wake siyo mashahidi pekee wa tukio hilo, bali kuna ushahidi na mashahidi wengine ambao wangeweza kuhojiwa na wapelelezi lakini hawajahojiwa na wala taarifa yoyote ya uchunguzi kutolewa.

“Jeshi la Polisi halijawahoji majirani zangu nyumbani kwa Waziri wa Nishati Medard Kalemani, Mbunge wa Ulanga Magharibi, Haji Mponda na Katibu Mkuu. Hawa nilikuwa naishi nao kwenye jengo moja.

“Jeshi la Polisi halijawahi kueleza nani aliyeondoa CCTV iliyokuwapo kwenye jengo la makazi yangu baada ya shambulio; kwa nini iliondolewa; mahali ilikopelekwa, na ni kitu gani kinaonyeshwa kwenye CCTV hiyo,” amesema Lissu anayeendelea na matibabu nchini Ubelgiji.

Lissu amesema: “Jeshi la Polisi halijawahi kueleza hata aina ya silaha au risasi zilizotumika kunishambulia, taarifa ambazo hazihitaji uwapo wangu, bali uchunguzi wa kitaalamu wa silaha.”

Katika maelezo yake, Lissu amesema: “Kwa hiyo, katika mazingira haya, kauli ya Balozi Possi kwamba uchunguzi wa shambulio dhidi yangu unasubiri mimi na dereva wangu turudi Tanzania, ni kauli ya kukwepa kuwajibika kwa vyombo vya upelelezi vya Serikali ya Tanzania.”
Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com