Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk Abdallah Possi ametoa tamko akijibu madai ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyoyatoa hivi karibuni nchini humo alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha News Africa cha kituo cha televisheni cha Deutsche Welle (DW).
Lissu ambaye kwa sasa yuko nchini Ubelgiji akiendelea na matibabu kufuatia shambulio la risasi la Septemba 7, 2017 jijini Dodoma amekuwa akiituhumu Serikali kuhusika huku akihoji sababu ya kutokamatwa kwa mshukiwa yeyote, mbali pia na madai ya ukandamizwaji wa demokrasia nchini.
Akijibu madai ya Lissu katika tamko lake la Januari 29, 2019, Dk Possi amesema Serikali imekuwa ikilifuatilia suala hilo ikiwa ni pamoja na kuanza uchunguzi.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa taarifa ya kulaani tukio hilo na kuagiza uchunguzi wa kina wa haraka. Kwa nyakati tofauti Rais amemtuma Makamu wake, Rais mstaafu na viongozi wengine wa Serikali kumtembelea Lissu akiwa hospitali akiwa Dodoma, Nairobi na Brussels (Ubelgiji).”
“Ni vema sasa mbunge angepima ishara hizo njema za Rais kwenye madai anayotoa yasiyo na msingi,” amesema Dk Possi katika tamko lake.
Kuhusu madai ya kutochunguzwa kwa tukio hilo, Dk Possi amesema mamlaka za Serikali zingetaka kumpata Lissu ili atoe ushirikiano wa taarifa kuhusu tukio hilo.
Ameongeza uchunguzi ulishaanza mara tu baada ya tukio hilo lakini umeshindwa kuendelea kwa sababu ya kutopata ushirikiano kutoka kwa mbunge huyo.
Na Elias Msuya, Mwananchi